Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amewataka Maofisa Ugani waliopo mkoani hapa kujenga tabia ya kuwatembelea wakulima wa zao la muhogo, ili waweze kutoa elimu ya namna ya uzalishaji wa zao hilo.
Ndikilo ametoa wito huo juzi wakati akifungua kikao cha wadau wa zao la muhogo, kilichofanyika mjini Kibaha kilichoandaliwa na Chama Cha Wadau wa Zao la Muhogo (TACAPPA).
Amesema zao la muhogo ni moja ya zao muhimu na kwamba likitumika vizuri, linaweza kuwaongezea wakulima kipato na hata kuongeza kipato cha mkoa na pia kujenga uchumi wa taifa.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema wakulima wengi, wanalima zao hilo huku wakiwa hawana utaalamu wala elimu ya kutosha juu ya zao hilo na kwamba ni wakati wa Maofisa Ugani, kuona namna ya kuwatembelea wakulima kwa kuwapa elimu ya zao hilo.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Pwani, una jumla ya hekta 3,353,900 ambapo eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 1,933,224 sawa na asilimia 57.66 ya eneo lote.
Ndikilo amesema pamoja na kuwepo kwa ukubwa wa eneo hilo lakini bado muhogo, hulimwa kwa kiasi kidogo ikiwa ni wastani wa hekta 60,703 na kuzalisha tani 500,000 hadi 650,000 kwa mwaka huku akisema, eneo hilo ni asilimia tatu.
Kuhusu usindikaji, Mkuu huyo wa Mkoa amesema bado mkoa haufanyi vizuri pamoja na kuwepo kwa juhudi za kuanzisha vikundi na viwanda vya usindikaji, kwani vikundi 32 vilivyopo katika mkoa huo havisindiki mihogo kwa madai ya kukosa soko la uhakika.
Kwa upande wale Mwenyekiti wa TACCAPA Mwantumu Mahiza, amesema endapo wakulima watahamasishwa kuhusiana na zao hilo litawasaidia kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Mwantumu amesema Maofisa Ugani, wanatakiwa kusaidia kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima zao hilo kitaalamu na kupata mbegu bora na kwamba bila hivyo, hakuna mafanikio yatakayopatika.
Amesema chama hicho, kimejipanga kupambana na vikwazo vya soko la zao hilo ambapo vikitolewa wakulima watachangia kuinua uchumi wa taifa na kuondoa umaskini wa kaya.
Mwenyekiti huyo amesema, kwa sasa TACCAPA ipo katika mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha muhogo ambacho kitahudumia Mikoa ya Kanda ya Mashariki na Kati na kufanya zao hilo kupata soko kubwa zaidi.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Dkt. Dolphine Magere amesema kikao hicho kinalenga kutoa dira ya kuhakikisha zao la muhogo, linapata hadhi kama mazao mengine.
Magere amesema baada ya kikao hicho, timu mbalimbali kupitia halmashauri zitaundwa kwa kuwashirikisha Maofisa Ugani, ili wawe karibu na wakulima wa zao hilo.
Mmoja wa wakulima aliyeshiriki kikao hicho, Gosbert Joshua ameomba kuwepo na kituo cha kuzalisha mbegu za muhogo, ili kuondoa usumbufu wa kuzifuata mbali na wanapoishi.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito