March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Ugani Nkasi wahimizwa kuimarisha kilimo

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi

Maofisa Ugani wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa,wametakiwa kuendelea kutoa elimu ya kilimo cha zao la ufuta na mbaazi kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika na Kata nyingine zilizofanyiwa utafiti kwa ajili ya kilimo cha mazao hayo.

Wito huo umetolewa na Ofisa Kilimo,Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Dkt.John Tlatlaa, katika kikao kazi cha maandalizi ya msimu wa kilimo kwa mwaka 2025/2026, kilichofanyika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Novemba 20, 2025.

Dkt.Tlatlaa amesema kuwa Halmashauri hiyo imekusudia kuendeleza zao la ufuta na mbaazi kutokana na fursa za masoko ya mtandao uliopo.

“Kutakuwa na mashamba darasa takribani 39 kwa maeneo yote ya kata za mwambao ambayo yataanzishwa kwa mwaka huu kwa mazao ya ufuta,hivyo maofisa kilimo wa kata hizo katika maeneo yenu endeleeni kutoa elimu kwa watu kuweza kulima na kuandaa mashamba kwa ajili ya zao la ufuta,”amesema.

Sanjari na hayo amewataka maofisa kilimo hao kumsaidia Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,kukusanya mapato kupitia wafanyabishara wanaokwenda na malori kwenye maeneo yao kwa kuhakikisha wanalipa tozo zinazotakiwa.

Huku akiwahimiza kutosita kukagua malori hayo pamoja na kutoa taarifa kwa watendaji endapo watabaini kama hayajalipa ushuru ili Halmashauri ifikie malengo ya kufikisha huduma kwenye jamii.

Mkuu wa sehemu ya Kilimo,Emmanuel Gamasa,amesisitiza kuwa Maofisa Kilimo wote waongeze kasi ya usajili wa wakulima kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku pamoja na kuwashauri wakulima kwenye maeneo yao kutumia kanuni bora za kilimo.