Na Ashura Jumapili, TimesMajira online Kagera
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini Daniel Sillo amewaelekeza Maofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mikoa ya Kagera na Kigoma kuhakikisha wanafanya utambuzi, usajili na usambazaji wa vitambulisho hivyo kwa wananchi katika Wilaya, Kata na Vijiji haraka iwezekanavyo.
Wito huo ameutoa Agosti 10, 2024 akiwa mkoani Kagera kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika kwenye uwanja wa Mayunga Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Sillo, amesema kuwa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Serikali ilitenga bilioni 42.5 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa vitambulisho hivyo vya taifa ambapo kuanzia Oktoba 2023 vilianza kusambazwa nchi nzima.
Sillo, amemhakikishia Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM. )Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi, kuwa Mkoa wa Kagera kuna vitambulisho vya taifa 78,766 ambavyo havijakabidhiwa kwa wananchi hivyo amewataka Maofisa uandikishaji wote kutoka Wilaya zote kusambaza kadi hizo zilizoko tayari kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sillo, amesema Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Wakili Stephen Byabato, amekuwa akifuatilia kwa karibu kuhusu lini Serikali itaboresha majengo ya makazi ya Askari Polisi wanaoishi mtaa wa Buyekera Kata Bukoba.
Hivyo amesema Serikali kupita Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika mwaka wa fedha wa mwaka 2024/25 tayari wametenga kiasi cha bilioni 1 kwa ajili ya kujenga na kuboresha majengo hayo ya makazi ya Askali Polisi.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu