November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Elimu Mbeya wapewa agizo

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

MKUU wa Mkoa Mbeya, Albert Chalamila amewaagiza maofisa elimu Mkoani hapa kuweka mazingira rafiki kwenye Shule za Msingi na Sekondari yatakayowezesha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa watoto waliopo mashuleni.

Chalamila alitoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu duniani yaliyopewa Kauli mbiu ya ‘Sio kila ulemavu unaonekana’ ambayo katika Mkoa wa Mbeya yalifanyika katika viwanja vya shule ya watoto wenye ulemavu na wasio nao ambayo ipo chini ya Shirika la Child Support Tanzania (CST).

Kiongozi huyo ambaye aliwakilishwa na mMkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika amesema, hakuna haja ya kuwatenganisha watoto wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji kwani wote wanapaswa kujifunza kwa pamoja.

Amesema, baada ya kushuhudia namna shirika la CST lilivyofanikiwa kutoa elimu jumuisha kwa watoto bila ya kuwatenganisha likitumia mbinu za ubunifu ikiwemo ya kutumia vifaa vya kuchezea vinavyowafanya wanafunzi wenye mahitaji maalum wazingatie wakati mwalimu akiendelea kufundisha amevutiwa nao na kuona kuna haja maofisa elimu katika Mkoa wa Mbeya kuiga mfano na kujifunza kutoka shirika la CST na kuacha mfumo wa kuwabagua wanafunzi wenye mahitaji maalum mashuleni kwa kuwatenga kwenye shule zao au madarasa.

“Niwatake maofisa elimu na wengine katika shule zetu tuhakikishe tunaweza mazingira rafiki yatakayohakikisha watoto wetu kwa pamoja wanapata elimu kumuisha bila ya kuwatenganisha nadhani wakati tulipotembelea lile darasa kuna kitu mmejifunza,” alisema

Katika hatua nyingine Ntinika ameziagiza taasisi za umma na binafsi kuhakikisha zinatoa nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu kwani nao wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi kama watu wengine.

Amesema, hata ofisi yake ina watumishi wenye ulemavu na wanafanya kazi kwa bidii ukilinganisha na watu ambao hawana ulemavu wowote, huku akilipongeza shirika hilo kwa kuwa mfano wa kuwaajiri watumishi wake wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la CST, Noelah Msuya ameiomba serikali kufikiria kuanza kutoa elimu ya lugha ya alama kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la awali ili miaka ijayo Taifa lisiwe na uhaba wa walimu wa lugha hiyo.

“Jamii bado ina uelewa duni na mitazamo hasi kwa watu wenye ulemavu na jamii jumuishi nadhani ni kitu ambacho tunapaswa kuendelea kukipigia mbinja ili watu wengi zaidi waelewe lakini pia serikali itusaidie kuihamaisha jamii ishiriki kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao za msingi katika jamii,” alisema