November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Manusura achaguliwa kwa mara nyingine kuwa Naibu Meya Ilemela

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Diwani wa Kata ya Buzuruga Manusura Sadick amechaguliwa kwa mara nyingine kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.

Ikiwa ni mara ya tano mfululizo kushika nafasi hiyo baada ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Agosti 2,2024 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga,akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 kilichoenda sambamba na uchaguzi wa Naibu Meya, ameeleza kuwa jumla ya kura 27 za ndiyo sawa na asilimia 100 zimepigwa kwa ajili ya kumchagua Naibu Meya huyo.

Hata hivyo baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo wameeleza sababu mbalimbali zilizowafanya wakamchagu Manusra kwa awamu ya tano mfululizo.

Diwani wa Kata ya Pasiansi Rosemary Mayunga, ameeleza kuwa wamemchagua kwa mara ya tano kwa sababu ya mafanikio ambayo wamekuwa wakiyapata katika shughuli za maendeleo kwa Halmashauri hiyo na Kata zao.

“Kutokana na mafanikio kwenye uendeshaji wa miradi mbalimbali,tumeona kuna haja ya kumrudisha kwa sababu kulikuwa na miradi kiporo tunatarajia atafanya jitihada miradi hiyo ambayo imejengwa kwa nguvu za wananchi na mingine ilioanzishwa na mifumo ya serikali akamilishe kazi aliyokuwa ameianza,”ameeleza Rosemary.

Hivyo wanaamini mpaka kumaliza kipindi chao cha udiwani watakuwa wameisha kamilisha miradi ya maendeleo ikiwemo afya,elimu, miundombinu,maji na kadhalika.

Diwani wa Kata ya Buswelu Sarah Ng’hwani, ameeleza kuwa Naibu Meya huyo ni mtu asiye kuwa na longolongo na ana ushirikiano na Madiwani wenzake.

“Kila tukimpelekea hoja zetu anatusaidia,anatekeleza miradi na fedha za miradi kwenye Kata zetu,hana janja janja ya kuwa na makundi,ukimueleza jambo hata kama una shida ya dharura anakusikiliza,na sisi Madiwani tupo kama watoto wadogo uwa tunapenda kukimbiliwa unapoona mwenzio anakukimbilia basi huyo ndio kiongozi,”ameeleza Sarah.

Diwani wa Kata ya Kitangiri Donald Ndalo, ameeleza kuwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wameridhishwa na utendaji kazi wa Naibu Meya huyo tangu awamu ya kwanza mpaka sasa.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri hiyo Manusura Sadick, ameeleza kuwa kushinda nafasi hiyo kwa miaka mitano mfululizo siyo jambo dogo bali ni uaminifu kutoka kwa Madiwani.

Ameeleza kuwa kitu anachojivunia katika kipindi cha miaka minne ni usimamizi wa fedha za serikali kuu pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri.

“Nimekuwa mkali katika kusimamia fedha zinazokuja,pia namna ya kuwasilisha mawazo katika kuleta maendeleo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,tumejenga tumejenga vituo vya afya vitatu, zahanati zaidi ya nane kwa mapato ya ndani,shule za msingi na sekondari,tumeboresha vifaa tiba katika kipindi hiki cha miaka minne,”ameeleza Manusura na kuongeza kuwa;

“Tumeisha anza kumalizia maboma yote ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na juzi tumeidhinisha zaidi ya milioni 260 kwa ajili ya kwenda kukamilisha maboma hayo,nidhamu katika usimamizi wa fedha unaongeza imani kwa Madiwani wenzangu,”.