*Ni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa TACTIC
*Kata nane za Manispaa ya Moshi kunufaika na mradi huo
*Utekekalezaji wake ni wa miezi 15
Martha Fatael, Timesmajira Online-Moshi
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imesaini mkataba wa Shilingi bilioni 22 na kampuni ya ujenzi ya Hari Singh & Sons Limited ya mjini hapa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo barabara, mitaro na ujenzi wa jengo la wakandarasi.
Mikataba hiyo imesainiwa chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji nchini Tanzania (TACTIC), ambao utatekelezwa katika kata nane za Manispaa ya Moshi, ambazo ni: Njoro, Rau, Kiboroloni, Mjimpya, Shirimatunda, Pasua, Soweto na Ng’ambo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo iliyofanyika Septemba 27,2025,katika kata ya Ng’ambo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe,amesema mradi huo wa miezi 15 utaanza rasmi Oktoba Mosi,2025 hadi Desemba 31,2026.
Nasombe, amesema mradi huo utajumuisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13.25, pamoja na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 3.9, na jengo la ghorofa moja kwa ajili ya wakandarasi.
Ambapo barabara zitakazojengwa ni pamoja na barabara ya Ruwaichi–Njoro (km 6.9), barabara ya Pepsi (km 1.25) na
barabara ya Shirimatunda–Magereza (km 5.1).
Kwa upande wa mitaro ya maji ya mvua, itajengwa kutoka Ushirika hadi Moshi Pazuri (km 2.0) na mtaro wa Kinong’oto (km 1.9).

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI,Adolfu Ndunguru,amesema mradi wa TACTIC unatekelezwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya miji na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi.
Amesema mradi huo kwa unagharimu Dola za Kimarekani milioni 410 sawa na takribani tilioni 1.1,fedha ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu huyo, Mhandisi Emmanuel Manyanga amesema,mradi huo unatekelezwa katika miji 45 nchini kote, ambapo awamu ya kwanza tayari imeanza, na mikataba inayosainiwa sasa ni sehemu ya awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa TACTIC.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Nurdin Babu, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa miradi hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama endapo kutatokea vitendo vya hujuma au wizi wa vifaa vya ujenzi.
“Mkoa wa Kilimanjaro umepokea jumla ya tilioni 1.4 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo, ambazo zimegawanywa kwa kila wilaya kulingana na mahitaji ya msingi,”amesema Babu.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi,Godfrey Mnzava,amesema kati ya mwaka 2021 hadi 2024, Serikali imewapatia zaidi ya bilioni 253 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo, ambapo Shilingi bilioni 93 zimeelekezwa kwenye sekta za elimu, afya na miundombinu.

Naye mkandarasi Amandeep Dhani kutoka kampuni ya Hari Singh & Sons Limite,ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wa ndani, hatua hiyo inaongeza imani na kuchochea maendeleo ya kampuni za wazawa.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Ng’ambo walioshiriki hafla hiyo, akiwemo Maria Shayo na Christen Singano, wameomba utekelezaji wa miradi hiyo ufuate viwango vya ubora kama vilivyoainishwa kwenye mikataba, wakikumbusha kuwa baadhi ya miradi ya nyuma ilijengwa chini ya kiwango na kuharibika mapema hasa wakati wa mvua.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi