November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Manispaa ya Kigamboni yaanza mchakato wa kuyatambua maeneo yaliyopo katika machimbo ya vifusi vya kokoto

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigamboni imesema kwamba imeanza mchakato wa kuyatambua maeneo yote yaliyopo katika machimbo ya uchimbaji vifusi vya kokoto yaliyopo Mbutu ili kuanza kwa mchakato wa ulipwaji wa fidia kwa wananchi wenye maeneo hayo.

Jambo hilo linafanyika ikiwa ni sehemu ya  utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo wakati alipofanya ukaguzi katika machimbo hayo nakutaka halmashauri kuyatambua rasmi maeneo hayo kama sehemu ya machimbo.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni mjini Kigamboni, Ofisa wa Idara ya Mazingira katika halmashauri hiyo, Juvenalis Mauna alisema serikali ipo katika harakati ya kuyatambua maeneo yote kwenye machimbo hayo ili mchakato wa ulipaji wa fidia uanze.

Alisema kinachofanyika sasa ni kuhakikisha eneo hilo lote la uchimbaji linakuwa maalum kwa shughuli za machimbo na kwamba idara ya madini ilifanikiwa kufika katika machimbo hayo na imeshawafungia leseni waliosababisha kutokea kwa ajali iliyoua watu watatu hivi karibuni.

“Kuna mambo mawili hapa katika suala la ulipaji fidia yanaweza kufanyika, kuna wale ambao watalipwa na kukubali kuondoka moja kwa moja na wapo ambao watayatoa maeneo yao kwa kampuni za uchimbaji ambao watawalipa na baadae wanarudishiwa maeneo yao, lakini ikumbukwe kwamba mchakato umeanza ila hauwezi kuisha kwa mara moja ” alisema

Asha Omary ni mkazi wa Mbutu na mchimbaji wa kokoto amesema licha ya Serikali kujipatia mapato kutokana na mradi huo wanaiomba kuiboresha barabara iliyopo katika machimbo hayo ili kupunguza fumbi linaliwapata kila siku.

“Licha ya uwepo wa fumbi, pia tunaiomba Serikali kutuletea maji na umeme katika eneo hili la Mbutu ambalo ni maarufu kwa utoaji wa vifusi vya kokoto ambavyo vinatumika kutekekeza miradi mikubwa ya serikali,  tunafahamu wanataka kuyatambua maeneo yote hivyo tuombe mchakato wa fidia kama upo basi ufanyika kwa haraka na wakati,” amesema.

Maeneo ya uchimbaji wa vifusi vya kokoto Kigamboni

Naye Mchungaji Stephen Mshana ambaye pia ni mchimba kokoto katika eneo hilo la Mbutu Kigamboni,  amesema eneo hilo kuna wakinamama wengi ambao na wao wanahitaji kupatia mikopo hivyo halmashauri iwakumbuke.

“Hapa kuna wakinamama wengi wanafanya kazi ya kuchima kokoto na kuziponda, ipo mikopo ya halmashauri ni vema na wao wakakumbukwa na kuangaliwa kwa jicho la tatu ili wasifanye kazi hii kwa muda mrefu,” amesema.

Akizungumza na mwandishi wa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkwajuni Kata ya Somangila wilaya ya Kigamboni,  Lucas Matemani amesema anaungana na wakazi hao kuiomba Serikali kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Dege Ngomvu ambayo inatumika kupitisha maroli makubwa yanayobeba kifusi hicho ili kuondoa fumbi katika makazi ya watu yaliyokaribu na barabara hiyo

Amesema zipo jitihada mbalimbali zimefanywa na wadau wa machimbo hayo kupunguza fumbi ikiwemo kumwagia maji barabara hiyo mara kwa mara na kuingia makubaliano ya kumwaga kifusi kisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kuleta mitambo kwa ajili ya kushindilia.

“Hapa kwa siku zaidi ya gari 500 zinapita, hivyo tumetoa maelekezo kila gari linalobeba kifusi linapaswa kumwaga kifusi kimoja cha kujitolea katika barabara hii ya Dege Mgomvu – Mkwajuni, lakini ili kuweza kuondokana na fumbi tunaomba Serikali iweze kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami,” amesema Matemani.

Aidha Matemani amewataka Tume ya Madini na wasimamizi wa mazingira wilayani humu kuhakikisha wanasimamia uchimbaji huo ili uzingatie sheria na taratibu za kimazingira zilizopo nchini.

“Tunaomba pia usimamizi wa machimbo haya uendelee kwa weledi  na kuthaminiwa ili kuepusha madhara ikiwemo vifo vinavyoweza kutokea kama watu hawatawajibika ipasavyo, pia mikopo itolewe kwa wakinamama wanaogonga kokoto kwani katika mtaa wangu tu zaidi ya Milioni 40 zimeshatolewa kwa makundi ya wanawake na vijana,” amesema.

Septembe 30, mwaka jana Waziri Jafo akiwa katika machimbo hayo hakufurahishwa na namna shughuli za uchimbaji zinavyofanyika kwani hazizingatii utunzaji na uhifadhi wa mazingira huku mmiliki wa machimbo hakufanya tathimini ya athari kwa mazingira na wala hana cheti cha mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jambo ambalo alisema ni kinyume na utaratibu.

Kufuatia changamoto hiyo, Waziri Jafo alimtaka mmiliki wa machimbo hayo kufanya tathimini ya athari kwa mazingira na kufika NEMC kujisajili kisha kupata cheti cha mazingira ili kuweza kuepusha madhara yanayoweza kutokea katika machimbo hayo na watu waendesha familia zao kwa kuchimba kokoto hizo.