December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Manispaa Tabora kutoa mikopo ya Bil. 1.45 kwa vikundi vya wajasiriamali

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya manispaa Tabora inatarajia kutoa mikopo ya kiasi cha sh bil 1.45 kwa vikundi vya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi baada ya serikali ya awamu ya 6 kuruhusu utoaji mikopo hiyo uendelee.

Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alipokuwa akifungua kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.

Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu zoezi la utoaji mikopo kwa ajili ya vikundi vya wananchi vinavyojishughulisha na ujasiriamali kuendelea kutolewa na halmashauri zote nchini baada ya kusitishwa kwa muda.

Ameisitiza kuwa utaratibu wa utoaji mikopo hiyo umeboreshwa na kila kikundi kitakachokopeshwa fedha hizo kinapaswa kuzirejesha pasipo riba yoyote kama ilivyokuwa awali.

‘Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuruhusu mikopo hii ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri kuendelea kutolewa kwa vikundi vya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu ili kuwakinua kiuchumi’, amesema.

Mstahiki Meya amesisitiza kuwa hizo hela sio za bure, kila kikundi kitakachokopeshwa ni lazima kihakikishe kinazirejesha kwa wakati ili vikundi vingine vikopeshwe.

‘Kuanzia sasa tutahakikisha kikundi chochote kinachohitaji kuchukua mkopo huo kina biashara ya kueleweka na kina uwezo wa kuurejesha, vinginevyo hakitapewa, tayari Wataalamu wameshaanza kupita mitaani kukagua vikundi vyote’, ameeleza.

Amewataka Wataalamu wa manispaa hiyo kusimamia ipasavyo mikopo hiyo na kufuatilia vikundi vyote vitakavyokopeshwa ili kuhakikisha fedha wanazopewa hazitumiki kinyume na utaratibu na wahakikishe zinarejeshwa kwa wakati.

Aidha Mstahiki ameagiza Wataalamu kuhakikisha fedha zote zinazoletwa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo zinasimamiwa ipasavyo ili zifanye kazi iliyokusudiwa kinyume na hapo halmashauri itawachukulia hatua stahiki.

Amempongeza Mkuu wa Idara ya elimu sekondari kwa kusimamia vyema ufundishaji katika shule zote hali iliyopelekea shule ya sekondari ya Wavulana Tabora kufanya vizuri sana Kitaifa katika mitihani ya kidato cha 6 mwaka huu.