Na Dotto Mwaibale,Timesmajira Online. Singida
MADIWANI na Wakuu wa Idara wa Manispaa ya Singida, wamepatiwa mafunzo ya siku juu ya kifua kikuu (TB) na UKIMWI kwa watoto kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Mafunzo hayo yametolewa na Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA) kupitia mradi wa CAP TB-Singida kwa ufadhili wa EGPAF, unaohusisha Mikoa ya Tabora na Singida katika kukabiliana na tatizo la TB na UKIMWI kwa watoto.
Akizungumza jana katika mafunzo hayo mratibu wa mradi huo wa mikoa hiyo, Sadam Kidera amesema bado kuna imani potofu miongoni mwa jamii kwamba mtoto anapougua magonjwa hayo anaonekana kuwa amerogwa.
Kutokana na hali hiyo, amesema watoto wanapobainika kuugua maradhi hayo ni vyema jamii ikachukua hatua za kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, badala ya kuamini imani za kishirikina.
“Ni vyema na jukumu letu kuwafikishia wananchi na jamii kwa ujumla umuhimu na kutambua kwa kina zaidi kwamba ni suala la muhimu na msingi, waweze kuchukua tahadhari na elimu kutolewa jinsi gani ya kupata matibabu,” amesema.
Kidera amesema magonjwa hayo ni hatari, hivyo ni vyema jamii ikachukua hatua ya kukabiliana nayo mapema kwa kuwa yanatibika.
Kwa upande wake Katibu wa Mkuta Mkoa wa Singida, Michael Moses amesema jamii inapoona dalili za watoto wao kuugua kifua kikuu na UKIMWI inapaswa kuwapeleka mara moja kwenye vituo vya kutolea tiba, tayari kwa ajili ya kupatiwa matibabu sahihi.
Mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mkoani Singida kuanzia Juni, 2020 na kufikia tamati Juni mwaka huu utaiwezesha jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na magonjwa hayo.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi