Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MAMENEJA wa Mikoa wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wametakiwa kuhakikisha barabara zote zilizoko katika maeneo yao ya kiutawala zinapitika wakati wote ili kuwaondolea kero wananchi na kurahisishia utekelezaji shughuli za maendeleo.
Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokuwa akifungua Mkutano wa 18 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS uliofanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini Tabora.
Alisema serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa sana ya kuwatumikia wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara na miundombinu yake katika Mikoa yote nchini.
Alipongeza watumishi wa Wakala huo walioteuliwa kuwa Mameneja katika Mikoa mbalimbali na kuwataka kutambua kuwa nafasi walizopewa sio zawadi bali ni dhamana ya kuwatumikia wananchi, hivyo akawataka kuonesha weledi wao.
‘Tumieni dhamana mliyopewa kwa manufaa ya wananchi, hakikisheni barabara zote zilizopo katika maeneo yenu ya kiutawala zinapitika wakati wote, endeleeni kutoa huduma bora kwa wananchi katika kipindi hiki cha mvua’, alisema.
Naibu Waziri aliongeza kuwa Kurugenzi ya Manunuzi inakamilisha hatua za ununuzi wa Makandarasi kwa miradi ya kimkakati na mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo itasainiwa mapema iwezekanavyo katika robo ya kwanza ya mwaka.Aidha aliwataka kuhakikisha fedha zilizotengwa kugharamia ziara za mafunzo zinatumika kama zilivyopangwa ili kuwajengea uwezo na uzoefu watumishi wa Wakala huo kutoka katika miradi ya nchi nyingine inayofanana na ya kwao.Katika kuhakikisha miundombinu ya barabara zinazojengwa na serikali haiharibiwi, aliagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwasaka na kuwachukulia hatua wale wote wanaoharibu au kuiba alama za barabara ikiwemo kudhibiti mifugo inayopitishwa barabarani.Naibu Waziri aliwapongeza wafanyakazi kwa kufanikisha mkutano huo muhimu na kubainisha kuwa utawajengea ukaribu wa kiutendaji na kuaminiana kati ya Wafanyakazi, Chama chao na Menejimenti, na hiyo ndio chachu ya ufanisi wao.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatus Mativila alimhakikishia Naibu Waziri kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi wenye kuleta tija kwa thamani ya Fedha zinazotumika kwenye miradi ya ujenzi wa barabara.Alisema wataendelea kupokea na kufanyiwa kazi maelekezo watakayopewa na serikali ili kutimiza matarajio ya Watanzania ya leo na kesho.
Alisisitiza kuwa licha ya uwepo wa changamoto kadhaa za kiutendaji, anaamini Wizara itaendelea kuzifanyia kazi kwa ukaribu na pengine kuzimaliza kabisa katika kipindi cha muda mfupi.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua Baraza hilo, Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alimpongeza Rais Samia kwa kupelekea mabilioni ya fedha za ujenzi wa barabara za lami katika Mkoa huo ikiwemo kuwekwa taa za barabarani na za kuongozea magari, mkoa sasa unang’ara na ulinzi umeimarika.
Alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Wajumbe wa Baraza hilo kuja kuwekeza katika Mkoa huo au kujenga nyumba za makazi kutokana na fursa lukuki zilizopo ikiwemo usafiri wa uhakika wa ndege, barabara na reli.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato