Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
Mama lishe jijini Mbeya,wamehimizwa kugeukia matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi,ili kupunguza matumizi ya mkaa na kutunza mazingira.
Wito huo,umetolewa Septemba,30,2024 na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) mbaye pia ni Spika wa Bunge , Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson,wakati aliposhiriki mapishi na mama lishe, stendi ya Usangu mtaa wa Sokoni Kata ya Igawilo,jijini Mbeya.
Dkt.Tulia amesema, matumizi ya nishati ya gesi yataokoa muda na mazingira katika maeneo mbalimbali nchini hususani ukataji miti na mkaa ambao umekuwa ukiharibu mazingira.
Meneja miradi wa Nishati safi ya kupikia wa kampuni ya Oryx Tanzania,Peter Ndomba, amesema,wamekuwa wakihamasisha jitihada za matumizi ya nishati mbadala, kwa kufikia zaidi ya asilimia 80 kwa miaka 10.
“Hapa tumeona,mama lishe wakitumia mkaa,sasa ili kuwaambia kuwa gesi inawezekana,, imebidi Dkt.Tulia,apike mwenyewe ikiwa ni mfano halisi wa matumizi wa nishati hiyo,”amesema Ndomba.
Ndomba amesema kampuni ya Oryx,imepata faraja kuona kiongozi mkubwa ameamua, kuwa mfano kwa wananchi na kuacha alama ya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya gesi ya kupikia.
Hata hivyo,amesema tangu zoezi hilo limeanza mpaka sasa, wameweza kutoa mitungi zaidi ya 70,000 kwa jamii mbalimbali, hususani mama lishe na baba lishe, ambao kila siku wapo kwenye kuni na mkaa.
Ambapo ameeleza kuwa maisha ya watanzania wanaotumia nishati ya kuni na mkaa yapo hatarini,huku akisisitiza kuwa zaidi ya watu 33,000 hufariki kila siku kutokana na matumizi ya nishati hizo ambazo siyo safi,hivyo kuanza na kundi hilo wanaamini wanaweza kuokoa kundi kubwa la wananchi.
Kwa upande wake mmoja wa mama lishe, Joyce Mapunda, amesema kuwa toka alipoanza matumizi ya nishati safi ya gesi ya kupikia,ameweza kujifunza vitu vingi ikiwemo utunzaji wa mazingira,pamoja na kuokoa muda ambao anatumia katika shughuli nyingine za uzalishaji mali tofauti na utumiaji wa kuni.
Huku akiomba nishati hiyo kupunguzwa bei,ili watu wengi waweze kutumia na kutunza mazingira.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria