December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mama aliyetekeleza watoto kwenye majaruba akamatwa

Judith Ferdinand, Mwanza

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limemkamata mwanamke mmoja kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kutelekeza watoto wawili lililotokea Aprili 27 mwaka huu, saa 11 alfajiri katika mashamba ya mpunga (majaruba).

Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Happiness Mafuru mwenye umri wa miaka 23 mkazi wa Nyamhongolo Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza, aliwatelekeza watoto hao katika mashamba hayo yaliyopo mtaa wa Mtakuja.

Akizungumza tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP.Muliro Jumanne, amesema mwanake huyo alikamatwa Nyakato Wilayani Ilemela kwa tuhuma za kuwatelekeza watoto hao waliofahamika kwa majina ya Kelvin Mathias mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba pamoja na Anastazia Mathias mwenye umri wa miezi minne.

ACP.Muliro alisema watoto hao wanaendelea vizuri katika hospitali ya Rufaa ya Bugando huku jeshi hilo likiendelea na upelelezi wa kina ili kujua mazingira ya tukio husika yakoje ikiwa ni pamoja na kuendelea kumsaka mzazi mwenzake aliyetoroka baada ya tukio hilo.