Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa gharama za matibabu kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa ambayo uchangia uchumi wa familia kushuka.
Huku yakisababisha madhara katika maeneo mbalimbali ikiwemo kimaisha, kiuchumi,kiafya,kijamii na kusababisha vifo vya mapema kwa watu wengi.
Hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima,ametoa wito kwa jamii kujenga tabia ya kupima magonjwa ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya uwepo wa maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza,kupima afya zao ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Mwanza kuanzia leo Novemba 5 huku kilele kikiwa Novemba 12 katika uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Malima ameeleza kuwa, athari za magonjwa hayo katika mfumo wa maisha na kiuchumi ni kubwa sababu mapato ya mtu yanatumika kugharamia matibabu (kujitibu) huku mwili ukiwa dhaifu kwa baadhi kukatwa viungo vya mwili.
Ameeleza kuwa suluhisho la ukubwa wa gharama hizo za matibabu ni kupima afya mapema na kupuuza misemo kuwa kupima ni kumchokoza Mungu,watu wasiyachukulie poa na bla bla maadhimisho.
“Wakati maadhimisho haya yenye kauli mbiu ya “Badili mtindo wa naisha boresha afya yanafanyika takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la wagonjwa kutoka watu milioni 4 mwaka 2018 hadi kufikia milioni 4.8 mwaka 2022, ongezeko hilo linaathiri afya ya mtu mmoja mmoja,jamii na uchumi kwani matibabu yake yanagharimu fedha nyingi,”ameeleza Malima.
Sanjari na hayo,Malima ametoa wito kwa wataalamu wa afya kutumia maadhimisho ya mwaka huu kutoa elimu na mbinu kwa wananchi ya kuyaepuka na kuyakabili magonjwa hayo.
“Mtu anayeshindwa kuchukua tahadhari ubora wa maisha yake unakuwa katika changamoto, elimu itolewe ili wananchi wachukue hatua ya kupima mara kwa mara badala ya kusubiri hadi waugue ambapo madhara yameshakuwa makubwa,”.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) Dkt.Happy Nchimbi ameeleza kuwa wakati maadhimisho ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha magonjwa hayo yanaongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote kimaisha, kiuchumi, kiafya na kijamii.
“Takwimu za WHO za mwaka 2016 zinaonesha magonjwa hayo ya shinikizo la juu la damu, kisukari,saratani,pumu,magonjwa ya afya ya akili na selimundu yanachangia zaidi ya vifo milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea katika mwaka huo,pia magonjwa hayo yanachangiwa na vihatarishi vinavyofanana na vinatokana na tabia na mtindo wa maisha,”ameeleza Dkt.Nchimbi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) Prof. Andrew Swai wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari Jijini Mwanza, ameeleza kuwa wagonjwa wa magonjwa hayo wanaongezeka kila Mwaka kutokana na mtindo mbaya wa maisha kwa kutozingatia vyakula pamoja na kutojishuhulisha na jambo lolote (hali inayopelekea kuwa na tabia bwete.
“Mazoezi ni muhimu sana angalau ufanye nusu saa kwa siku hii itasaidia utokwe na jasho ambalo hupunguza chumvi mwilini na kusaidia kutopata magonjwa hayo kama kisukari, saratani na shinikizo la damu, usikae siku nzima bila kufanya zoezi,”ameeleza Prof. Swai.
Prof. Swai amewatahadharisha watanzania kupunguza kunywa vinywaji kama soda,juisi na vilevi kwani vyote hivyo hupelekea kupata magonjwa hayo akitolea mfano wa soda kuwa kawaida huwa na vijiko tisa vya sukari huku kiafya kwa siku mtu anashauriwa kutumia sukari isiyozidi vijiko 5.
Aidha Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(WHO) imesisitiza kuwa bado uelewa wa umma kuhusu uhusiano uliopo baina yamagonjwa yasiyoambukiza na hatari ya vichocheo vyake kama matumizi ya tumbaku na pombe , lishe duni na kutofanya mazoezi ni mdogo sana. Hivyo limezitaka nchi kuongeza juhudi katika upande huo pia.
Shirika hilo la afya linasema lengo kubwa ya ripoti ya sasa na wito wake ni kuhakikisha hatua zitakazochukuliwa zinaokoa maisha ya watu milioni 50 ifikapo mwaka 2030 kote duniani .
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba