January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Malezi mabovu yatajwa kuchochea ukatili kwa watoto

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Ukerewe

Imeelezwa kuwa,chanzo cha ukatili wa watoto unatokana na malezi mabovu kutoka kwa wazazi,hivyo ni jukumu la mzazi,kuwalea watoto katika misingi imara ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za maisha.

Hayo yamebainishwa na Agosti 28,2024, na Koplo Stella Liymo wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana,wakati wa ziara ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafugwa katika kisiwa cha Bwiro na Lyamwenge wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.Amesema ni jukumu la mzazi,kumuandaa mtoto kiakili,kimwili na kiroho.

Ambapo ameeleza hali hiyo itamsaidia mtoto kufahamu kuwa yupo katika ulimwengu gani?. Na namna gani hataweza kukabiliana na changamoto zilizopo katika ulimwengu huu.

Sanjari na hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, akizungumza na wananchi wa Visiwa vya Bwiro na Lyamwenge,amesema jukumu la kuzuia uhalifu ni la umma.Hivyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.

“Viongozi na wananchi wa visiwa hivi, kuhakikisheni hamuruhusu maeneo haya, kuwa sehemu ya wahalifu kujifichia, badala yake toeni taarifa Polisi kwa hatua zaidi za kisheria,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wenceslaus Muchunguzi,amewahimiza wakazi wa visiwa hivyo, kuhakikisha wanavaa vifaa vya kujiokolea kabla ya kuingia ziwani,ili kuepukana na vifo vitokanavyo na ajali za majini.

Baadhi ya wananchi wa visiwa hivyo vya Bwiro na Lyamwenge ,wameliomba Jeshi hilo la Polisi, kuendelea kutoa elimu, kwani itawasaidia kujiepusha na uhalifu na kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa Kamanda Wilbrod Mutafugwa na timu yake kutembelea maeneo yaliyoko pembezoni mwa Ziwa Victoria na visiwa vyake,ili kusikiliza kero, changamoto, malalamiko na kupata ushauri kwa wananchi sambamba na kufanya doria katika ziwa hilo.