November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makundi maalumu kupewa kipaumbele kupiga kura uchaguzi serikali za mitaa Lushoto

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Dkt.Ikupa Mwasyoge amesema wamejipanga kuona watu wote wenye mahitaji maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu wa macho na viungo vingine, wazee, wanawake wajawazito na wagonjwa, wanasaidiwa kupiga kura kwa haraka na kuondoka.

Lakini watu wengine watakaopewa kipaumbele cha kupiga kura na kuondoka, ni wasafirishaji wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, kwani katika watu waliohamasika kujiandikisha ni vijana ikiwemo wa bodaboda, hivyo wanatakiwa kufika ili kupiga kura, na kuwahi shughuli zao za kiuchumi.

Ameyasema hayo leo Novemba 26, 2024 wakati anazungumza na waandishi wa habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika kesho Novemba 27, 2024, na kuongeza kuwa maandalizi yote yamekamilika kwenye vituo vyote 1,005 vya upigaji kura kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi kwa ajili ya zoezi la upigaji kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika kesho Novemba 27, 2024. Zoezi litaanza saa mbili kamili asubuhi hadi saa 10 kamili jioni. Niombe sana muweze kufika, na hatutakuwa na mistari mirefu, na wala kutembea umbali mrefu sababu vituo vipo vingi.

“Lakini pia, watu wote wenye mahitaji maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu, wazee na waja wazito waweze kujitokeza kwa wingi kwa vile huduma zimekwisha kuandaliwa, na watapewa kipaumbele, lakini pia na waendesha bodabida nao watapewa kipaumbele ili waweze kupiga kura, na kuweza kuwahi kwenye shughuli zao za kujitafutia kipato” alisema Dkt. Mwasyoge.

Dkt.Mwasyoge alisema moja ya Tunu za Taifa ni amani yetu tuliyonayo hapa nchini, hivyo wananchi wote wanatakiwa kwenda kupiga kura kwa salama na amani na kuweza kurudi nyumbani kwa utulivu, kwani amani yetu ndiyo ushindi wetu, na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo sauti ya umma, hivyo wajitokeze kuchagua viongozi bora watakaowaongoza kwa miaka mitano.

“Amani yetu ndiyo ushindi wetu, na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo sauti ya umma, hivyo tujitokeze kuchagua viongozi bora ambao watatuongoza kwa miaka mitano, na kuweza kusimamia yale maendeleo makubwa tunayoyaona ambayo yanatolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo tupate viongozi bora, na tujiepushe na rushwa” alisema Dkt. Mwasyoge.

Dkt. Mwasyoge ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, alisema halmashauri yake ina majimbo mawili, Jimbo la Lushoto na Jimbo la Mlalo, na huko kote walifanya michezo na mabonanza mbalimbali ili kuwashawishi vijana katika kujiandikisha na kupiga kura, hivyo anaamini kutokana na kuwa na vituo vingi vya kupiga kura, na hamasa iliyofanyika, watu wengi ikiwemo vijana ambao ni wengi kwenye halmashauri hiyo, watajitokeza na watapiga kura  kwa wingi.