December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makumbusho ya Taifa kuongeza watalii, kudumisha utamaduni

Na Jackline Martin,TimesMajira Online

MAKUMBUSHO ya Taifa imejipanga kutumia njia mbalimbali za kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi kwa lengo kuongeza mapato ya taasisi hiyo pamoja na kuendelea kudumisha tamaduni za Kitanzania kwa ustawi bora wa Taifa.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Luoga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu onesho maalumu la Sanaa Pamoja Utalii Endelevu lililoandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya Nafasi Art Space litakalofanyika Mei 27, mwaka huu Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es salaam.

Onesho hilo linalenga kuwawezesha wasanii wa sanaa za ufundi na jukwaani kwa kuwapa fursa ya kutumia jukwaa na eneo la makumbusho kufanya kazi zao

“Programu ya Museum Art Explosion inaendana na Lengo la serikali ya kuhamasisha utalii wa utamaduni hivyo kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kazi kubwa ya Royal Tour,” alisema Luoga

Aliongeza kuwa Kazi ya Royal Tour ni kufungua fursa mbalimbali za utalii nchini Tanzania na wao kama Makumbusho ya Taifa wanaichukulia kama fursa ya kutangaza utalii wa asili na utamaduni.

Pia Luoga alisema katika mpango mkakati wa miaka mitano wa Taasisi yao 2021/22-2025/26 wana mpango wa kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi na kuongeza mapato ya Taasisi.

Kwa upande wake Mratibu wa Sanaa za Jukwaani kutoka Nafasi Art Space, Kwame Mchauru alisema katika tukio hilo kutatanguliwa na Mdahalo kuhusu kazi ya Sanaa kabla ya uzinduzi wa Kampeni ya Sanaa Pamoja ambayo itakuwa ikiendelea mwaka mzima kwa lengo la kuchangia ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Wananchi wa Mataifa ya Afrika.

Kupitia mradi huo wa Sanaa pamoja pia wanaangalia njia mbalimbali za kiubunifu zenye kukutanisha taaluma mbalimbali za kisanii pamoja ili kuunda Jumuiya ya Wabunifu inayosukuma maendeleo ya kazi mpya.