Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Rukwa
MKUU wa Mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere ameziagiza taasisi na kaya zote za mkoani humo kuhakikisha wanazingatia usafi na afya.
Makongoro ametoa kauli hiyo Julai 22,2024 ofisini kwake wakati wa mahojiano malumu na timu ya kampeni ya Mtu ni Afya, Fanya Kweli Usibaki Nyuma.
‘’Kwa kutambua, umuhimu wa afya, nakubaliana na kampeni ya Mtu ni Afya,Fanya Kweli Usibaki Nyuma natoa maagizo tisa kuhusiana na afya na ifikapo Oktoba 22 mwaka huu yawe yametekelezwa,,’’ amesema Makongoro.
Amesema agizo la kwanza,ni kila kaya na taasisi zote za Mkoa wa Rukwa kuwa na choo bora na kiwe kinatumika.
‘’Agizo la pili,kila kaya na taasisi iwe na kifaa cha kunawia mikono na kuzingatia kunawa kwa maji tiririka na sabuni katika nyakati malumu,’’amesema.
Katika agizo la nne, Makongoro ameagiza kila taasisi na kaya kufanya usafi wa maeneo ya makazi yao huku agizo la tano ni kila mwananchi wa Rukwa awe anafanya mazoezi ya mwili kila siku kwa dakika 30.
Agizo la sita kila kaya kuzingatia masuala ya hedhi salama pamoja na la saba ni kaya zote ziwe zinazingatia lishe bora.
‘’Ombi langu la nane ni kaya zote ziwe na utaratibu wa uaandaji wa maji safi na salama ya kunywa na ombi la tisa kila kaya izingatie matumizi sahihi ya nishati safi,”. amesema.
Katika hatua nyingine, Nyerere ameagiza kupewa taarifa ya kila wiki juu ya utekelezaji wa agizo hilo.
Naye Ofisa Afya Mkoa wa Rukwa, Martin Emmanuel amesema mkoa huo una tekeleza kampeni ya Mtu Ni Afya na kwa sasa wanasimamia ujenzi na matumizi ya vyoo bora.
‘’Mpaka sasa Mkoa wa Rukwa tuna asilimia 83 ya kaya zenye vyoo bora na bado tunaendelea na zoezi hili la ujenzi na usimamizi wa vyoo bora ili kuepuka wananchi kupata magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu,’’ amesema.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia