January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makonda kutomsahau Hayati Magufuli na Rais Samia katika safari yake ya siasa

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

KATIBU wa NEC ,Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda amesema hatamsahau Hayati John Magufuli na Rais Samia Suluhu Hassan katika safari yake ya kisiasa.

Pia amewataka wananchi wa Kanda ya Ziwa katu wasiwakilize watu wenye fitina wanaotaka kuwatenganisha Rais Samia na Hayati Magufuli,licha ya kuzaliwa Zanzibar,huku ni kwao.

Amesema Rais Samia kwa upendo wake ameleta fedha nyingi Kanda ya Ziwa kutekeleza miradi ya maendeleo,hivyo wana wajibu wa kumlinda, kumtetea na kumwombea afanye kazi kwa weledi.

Aidha ameagiza kufunguliwa kwa stendi ya mabasi ya Wilaya ya Sengerema ifikapo Novemba 13,2023 Jumatatu mchana ili iwahudumie wananchi huku akimtaka Mbunge wa Misungwi (CCM) Alexander Mnyeti,akamumombe radhi Charles Kitwanga ampe baraka.

Makonda ametoa kauli hiyo Novemba 12,mwaka huu kwa nyakati tofauti wilayni Sengerema, Usagara ( Misungwi) na jijini Mwanza baada ya kupokelewa akitokea Geita tayari kuanza ziara yake mkoani humu.

“Watu wanatumia fursa kuitenganisha Kanda ya Ziwa na Rais Samia,tusikubali katu Magufuli ndiye aliyemtambulisha, alikaa naye akaona uadilifu wake kuwa alimsaidia sana leo kuna watu wana mpinga,hata yeye (Samia) alisema ni kaka yake,hivyo ukimpinga, unampinga Magufuli,”amesema Makonda.

Pia amesema wananchi wa Kanda ya Ziwa wanapaswa kumtetea,kulimnda na kumwombea Dk.Samia,ana sifa za uongozi vinginevyo Magufuli asingempendekeza kuwa mgombea mwenza ingawa wapo watakaosema anayazungumza hayo kwa vile amenipa cheo na kusistiza asiwepo mtu Kanda ya Ziwa anayempenda Magufuli na kumchukia Rais Samia.

“Mimi siwezi kumsahau Magufuli naufahamu mchango wake katika safari yangu ya kisiasa na sitajifaragua sababu ya siasa,upo unafiki wa watu kujipendekeza hata wana siasa aliowapa uongozi leo wamemsahau Magufuli,Mama (Rais Samia) yupo kimya anafahamu iko siku pia watamsahau,”amesema Makonda.

Kuhusu hali ya nchi amesema kote alikopita amebaini mambo mawili, moja ni rushwa miongoni mwa watumishi wa umma na kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo kwa sababu ya kupiga (kuiba fedha) na kujengwa chini ya kiwango.

Katibu huyo wa NEC ya CCM amesema hilo si la Rais Samia bali la waliopewa dhamana ya kumsaidia hivyo ameziagiza kamati za siasa za Mikoa na Wilaya kufuatilia watumishi wazembe na wala rushwa na kuwachukulia hatua.

Amewataka wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kumuunga mkono Rais Samia,ana nia njema kwani hakuna mahali amekuta kuna tatizo la uhaba wa fedha isipokuwa rushwa na ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo ama kujengwa chini ya kiwango.

Kwa mujibu wa Makonda miradi yote aliyoanzisha Hayati Magufuli, Rais Samia ataitekeleza yote hakuna utakaobaki ambapo daraja la J.P Magufuli litakapokamilika litajenga uchumi wa nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema katika uongozi wa serikali ya awamu ya sita mkoa huo umepata sh.trilioni 1.4 za miradi ya maendeleo, ikiwemo ya ujenzi wa vivuko vine vipya, mradi wa mji Butimba na mingine mingi.

Amesema mradi wa daraja la J.P Magufuli umefikia asilimia 80,reli ya SGR na meli,itachochea uchumi wa wananchi na nchi za Afrika Mashariki zilizo katika ushoroba ambapo itajengwa bandari ya nchi kavu ya mizigo .