Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe kimewataka makada wa chama hicho na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwenye mapokezi ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda, anayetarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani hapa.
Ziara hiyo ya Makonda itakayohusisha mikutano ya hadhara pamoja na kusikiliza kisha kuzitafutia ufumbuzi kero za wananchi, inatarajia kuanza Februari 6 hadi 7, 2024.
Wakitoa taarifa ya pamoja Februari 2, 2024 Makatibu wa uenezi wa Wilaya za Momba na Ileje,Chuki Sichalwe na Maoni Mbuba, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za chama Mkoa zilizopo mjini Vwawa, Wilayani Mbozi , walisema makonda atapokelewa Februari 6, 2024 katika kijiji cha mkutano katika kata ya nzoka, Wilayani Momba akitokea Mkoani Rukwa.
“Katibu atapokelewa katika jimbo la Momba na moja kwa moja atakuja katika jimbo la Tunduma ambapo atafanya mkutano mkubwa wa kihistoria ikiwemo kupokea na kuzipatia utatuzi kero mbalimbali zitakazoibuliwa mkutanoni hapo” alifafanua chuki ambaye ni Katibu wa uenezi kutoka Wilaya ya Momba.
Amesema mkutano huo utafanyika majira ya saa nane katika shule ya msingi Tunduma.
Kwa upande wake, Katibu wa uenezi wa Wilaya ya Ileje, Maoni Mbuba, amebainisha kuwa Makonda ataendelea na ziara yake februari 7, 2024 katika Wilaya ya Mbozi kwa kufanya mkutano mkubwa katika Mji wa Mlowo na baada ya hapo ataendelea na ziara yake katika Mkoa jirani wa Mbeya.
Makonda amekuwa katika ziara kwenye mikoa mbalimbali kwa lengo kusikiliza kero za wananchi pamoja na kunadai mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu