January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makonda akunjua makucha, ampa Mchengerwa miezi mitatu 


Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Bukoba
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka mawaziri wa serikali ya Awamu ya Sita kujibu hoja mbalimbalii huku kikimpa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa miezi mitatu kutekeleza agizo la chama hicho kwa kufika mkoani Kagera ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
 
Maagizo hayo yametolewa leo na  Katiibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Paul Makonda  akiiwa katika ziara yake  mkoani Kagera kwa lengo la
kusikiliza na kutatua kero za wananchi ambazo kwa muda mrefiu hazijapata utatuzi.
 
Akizungumzia kero hizo ambazo ni pamoja na ujenzi wa soko usiokamilika, ujenzi wa stendi na kutatua changamoto ya mto Kanoni kwa kujenga kingo zake, Makonda amemtaka Waziri wa TAMISEMI kutafuta pesa ili kutatua kero hizo ambazo ziko nje ya uwezo wa wakazi hao.
 
“Waziri Mchengerwa nakupa miezi mitatu uwe umekanyaga Kagera, nataka kuona mpango wa ujenzi wa soko, tafuta pesa kokote soko lijengwe, nataka kuona stendi inajengwa Kagera, hiki siyo chama cha porojo” alisema Makonda
 
Akizungumza kwa njia ya simu na Makonda, Waziri Mchengerwa alisema amepokea maelekezo na ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na maelekezo ya Rais hivyo watatumwa wataalamu na kutekeleza maelekezo kama alivyoelekeza.
 
Waziri Mchengerwa aliahidi kuwa maelekezo hayo yatakuuwa yamekamilika kabla ya mwisho wa mwezi Desemba mwaka huu, na kuwa atafika Kagera na kuzungumza na wananchi, kukagua miradi yote na kuifanyia kazi.


Aidha Makonda amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kueleza hatua alizochukua kuhakikisha wananchi wanaoishi katika mipaka ya Mkoa wa Kagera wanapata vitambulisho vya taifa(NIDA).
 
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni alieleza kuwa Rais Samia alishalimaliza tatizo la upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ambapo tatizo kubwa lilikuwa ni malipo ya mkandarasi.
 
Akizungumza kwa njia ya simu Masauni alisema “hatukuwa tumemlipa mkandarasii ambaye ndio mzalishaji wa vitambulisho, katika bajeti yam waka uliopita ziilitengwa shilingi bilioni 42.5 ambapo zote zimeshalipwa”
 
Masuni alisema mpaka kufikia leo takwimu zinaonesha vitambulisho ambavyo vimeshaingia nchini ni takribani milioni 5, ikimaanisha jumla ya Watanzania milioni 16 wameshapata vitambulisho vya NIDA.
 
“Watanzania takribani milioni 22 tayari wana namba za utambulisho, na kufika mwezi wa 12, tutahakikisha kadi zote zimeshafika nchini na watu wote wamepata” aliongeza Masauni

Hata hivyo Makonda amemtaka Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa kutoa majibu kuhusu ujenzi wa kiwanja cha ndege, pamoja na ujenzi wa bandari ya mjini na Bandari ya Kemondo.
 
 Ambapo Waziri Mbarawa alisema ” Tutaanza kuweka taa katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba mwezi Februari 2023 kwaajili ya salama, pia kujenga jengo la kuongozea ndege (control tower) “
 
“Kwa upande wa Bandari ya Kemondo tayari mkandarasi ameshapatikana, tutakuja saiti muda wowote na kazi hiyo itachukua miezi 16 kukamilika, ambapo meli ya MV Mwanza ikianza safari rasmi, moja ya eneo litakalofunguk ni Bandari ya Kemondo na kukarabati Bandari ya Bukoba Mjini” aliongeza Mbarawa.
 
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya njia nne Bukoba, Makonda ametaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ambapo alisema tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 4 kwaajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
 
Katika hatua nyingine Paulo Makonda amewataka viongozi wa mashina na matawi kuendelea na vikao vyao vya kikanuni ili kuimarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi.
 
Katika ziara yake, Makonda amefika katika Ofisi ya CCM Mkoa na kusalimiana na wajumbe wa kamati ya siasa wa Mkoa, kisha kuzungumza na wazee wa Mkoa wa Kagera pamoja na Kamati ya Amani ya mkoa.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema wanaamini uwezo wa Katiibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,  Paulo Makonda wa kutatua changamoto za wananchi lakini pia kufikisha ujumbe kwa wenye mamlaka zaidi yake,
 
“Tunaamini zile kero atakazoondoka nazo Kagera zitafika juu, zitapatiwa ufumbuzi wa haraka na kuleta neema kwa wananchi wa Kagera” Amesema Mkuu wa Mkoa wa Kagera
 
Ameongeza kuwa kupitia mwaka wa fedha 2021/22 na 2023/24 wamepokea takribani Bilioni 477.18 ambapo kati ya hizo, Bilioni 225.9 ziliingia katika sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri zake, ambapo kupitia fedha hizo wamejenga madarasa ya shule za msingi 15, hospitali za Wilaya 8, vituo vya afya 12, zahanati 33, na bilioni nyingine 251, zimetumika kujenga barabara, maji na umeme.
 
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Steven Byabato, amesema Serikali ya Samia imewapatia shilingi bilioni 1 kwaajili ya kuanza ujenzi wa Stendi ya Bukoba mjini, bilioni zaidi ya 6 kwaajili ya marekebisho ya Uganda Road lakini pia upanuzi wa Bandari ya Bukoba Mjini ambapo Bilioni 18 zimetumika.
 
“Stendi tunayorekebisha sasa kwa ushirikiano wetu wote tumepata pesa ya kuanzia Bilioni 1, lakini ili tukamilishe tunahitaji takribani Bilioni 2 na Milioni 500 ambapo Bilioni 1 itatosha kujenga sakafu. Pia tunataka kujenga uzio na jengo zuri la ghorofa la abiria la kupokea na kuondoka”
 
Mmoja wa wakazi wa Chonyonyo, Wilaya ya Karagwe, Philimina Linus amesema yeye kama mawanamke ambaye amechaguliwa kuongoza Jukwaa la Wanawake katika Kata ya Chonyonyo aliushukuru uongozi wa Samia kwa kuwakumbuka wanawake na kuwapa mbinu nyingi za kujikwamua kwaajili ya kujiendeleza kiuchumi na familia zao kwaujumla
 
“Tunampongeza Rais Samia kwa  kuona mbali kumuinua mwanamke kwani mwanamke ndiyo nguzo kubwa katika uchumi wa nchi” amesema Philimina


Matukio mbalimbali katika picha