Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa wa kwanza kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuimairisha ulinzi na usalama kwa watalii mkoani humo kwa kutoa pikipiki 20 zenye thamani ya milioni 50 kwa Jeshi la Polisi.
Akizungumza Mei 16, 2024 kwenye hafla ya kumkabidhi pikipiki hizo iliyofanyika jijini Arusha, Makonda amesema pia benki hiyo imekuwa ya kwanza kutekeleza ahadi yake ya kutoa pikipiki hizo ndani ya mwezi mmoja kwenye uongozi wake mkoani hapo.
“Mmekuwa watu wa kwanza kwa mimi kutimiza ahadi zangu za kuimarisha ulinzi na usalama kwa watalii wetu wanaoingia mkoani Arusha. Niliomba msaada wa nyenzo ikiwemo magari kutoka taasisi mbalimbali na barua ya maombi kwa CRDB nimeitoa ndani ya siku saba tu leo mmetimiza ahadi yenu,” amesema Makonda na kuongeza kuwa
“Kwa namna nyingine, CRDB imemuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye safari hii ya kumlea mtoto utalii.Mtoto huyu amezaliwa na Rais kupitia Royal Tour, hivyo kwa kutoa pikipiki hizi, mtaimarisha ulinzi na usalama kwa watalii wetu,nataka kusema, bila usalama hakuna mtalii atakaeweza kuja nchini,”.
Makonda amesema anataka kuibadilisha Arusha kuwa Jiji la biashara na uchumi badala ya siasa, kwani nia yake ni kuona wananchi wanakuwa na kipato, huku akiwashawishi wananchi wapunguze kujenga fremu za biashara na badala yake wajenge vyumba vya kulala watalii kwani watapata pesa zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdulmajid Nsekela amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuongeza idadi ya watalii nchini kupitia filamu ya The Royal Tour, upatikanaji wa fedha za kigeni umeongezeka kwa Taifa na wananchi mmoja mmoja, hivyo wao kama benki, watawezesha wawekezaji kujenga hoteli mpya.
Nsekela amesema wanatambua sekta ya utalii ni kati ya maeneo muhimu yenye mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa, ajira za wananchi na ustawi wa jamii.
Sekta ya utalii inachangia asilimia 17.5 kwenye pato la Taifa na inaliingizia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni,mchango huo ni mkubwa unapaswa kuwekewa mikakati endelevu ili manufaa yake yakinufaishe kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema ili biashara na shughuli za utalii zifanyike kwa utulivu na uendelevu unaotakiwa basi ni muhimu kuwa na amani, utulivu na usalama katika Mkoa wa Arusha jambo litakalohakikisha maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii.
Kwa kuutambua umuhimu huo benki hiyo imekuwa ikishiriki na kutoa kipaumbele cha pekee kuimarisha usalama kwa kuchangia miundombinu na vifaa wezeshi vya kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu wa aina zote ili kuwawezesha wananchi kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii katika hali ya amani na utulivu.
“Hali hii ndio inayotufanya, wakati wote, tuwe tayari kuwezesha mikakati ya Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kulipa vitendea kazi kadri ya uwezo wetu ndio maana tulipopata ombi lako Mkuu wa Mkoa, tulilishughulikia kwa haraka tukiamini kuimarika kwa utalii mkoani hapa kutakuza uchumi na biashara yetu pia,”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi