December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makinda:Upatikanaji wa taulo za kike ni muhimu

Na Penina Malundo, timesmajira, Online

KAMISAA wa zoezi la Sensa na makazi ya watu ya mwaka 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amesema upatikanaji wa taulo za kike kwa wingi ni muhimu kwa maudhurio ya mtoto wa kike shuleni.

Makinda ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akipokea maaada wa taulo za kike kutoka kampuni ya Doweicare Technology kama sehemu ya kuunga mkono zoezi za sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

Amesema upatikanaji wa taulo za kike umuwezesha wanafunzi wa kike kuhudhuria shule kikamilifu na kupata haki yake ya msingi ya elimu sawa na vijana wa kiume.

“Taulo za kike ni afya ya kinamama na watoto wa kike, najua tuna mbinu zetu za kimila za kujihifadhi pale mtoto anapofikia umri fulani wakupata hedhi hata hivyo mbinu hizo zinaonekana kuwa siyo rafiki kwa sasa kwa wale wanaokwenda shule.

“Ndio maana zinapokuwepo taulo hizi za kike usaidia watoto waliopo mashuleni kuhudhuria kikamilifu masomo ya darasani na wanakuwa huru huku wakiondoa hofu, tunawashukuru Doweicare na Softcare kwa msaada huu ambao utakwenda kurejesha matumaini kwa wanafunzi wa kike waliopo katika shule mbalimbali nchini,” amesema 

Makinda ameitaka kampuni hiyo kufanya tafiti na kubaini maeneo gani yanachangamoto ya upatikanaji wa taulo za kike nakuweza kuwasaidia huku akiwasisitiza watanzania kuwa tayari kuhesabiwa katika Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Doweicare Technology,  Kenlyn Hu amesema wanashiriki zoezi la sensa kwa bidhaa zao za taulo za kike za Softcare kwenda kwa jamii ya kitanzania yenye uhitaji hususani wanawake.

alisema wanaamini kuwa mchango wao wa taulo hizo za kike zaidi ya 24,000 utahamasisha wanawake wa kitanzania kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa ili serikali kupata idadi sahihi ya watu kwa maendeleo ya nchi.

“Tunatambua na kupongeza Serikali ya Tanzania kupitia Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha wawekezaji na kutoa mazingira mazuri ya kufanya biashara ambayo yametengeneza fursa nyingi sana,”amesema