Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
KAMISAA wa sensa nchini na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda amesema matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yameisaidia serikali kufanya tathmini ya haraka kufuatia mafuriko ya matope wilayani Hanang mkoani Manyara.
Amesema tathmini hiyo imeirahisishia serikali kuwahudumia waathirika wa maafa hayo ya maporomoko ya matope ikiwemo kurejesha haraka huduma za kijamii ambazo ziliathirika na mafuriko hayo.
Ameyasema hayo Januari 29,2024 kwenye
Mafunzo ya uwasilishaji, usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi 2022 Kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Songwe.
Makinda amesema kwa kutumia taarifa za matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, pamoja na picha za ‘satelite’ serikali imeweza kufanya tathmini ya maafa hayo ambayo imesaidia kuweza kutoa msaada wa kiutu na makazi ya watu kwa urahisi.
“Waandishi ni wadau muhimu sana kwenda kuzitumia taarifa hizi mwenye shughuli zenu za kila siku,umuhimu wa matokeo hayo pia umeonekana kwenye maafa huko Hanang, serikali imeelewa haraka idadi ya mifugo na makazi ya watu namna yaliyoathirika na maafa,” amesema.
Amesema ni muhimu wanahabari kuacha kuandika taarifa za kusimulia ambazo hazina uhalisia, badala yake watumie matokeo ya sensa ya watu kufanya uchambuzi wa kina utakazozisaidia mamlaka kufanya uamuzi na kuchukua hatua.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Benno Malissa amewasihi washiriki wa mafunzo kwenda kuyatumia kama ilivyokusudiwa ili kuwa sehemu ya kuchochea maendeleo ya taifa.
Amesema matokeo ya sensa ya watu na makazi ni mwelekeo wa pekee utakaoliwezesha taifa kupanga mipango yake ya maendeleo, hivyo ni muhimu vyombo vya habari vikajiepusha na upotoshwaji wowote wa matokeo hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya, Nerbart Msokwa ameipongeza serikali kupitia ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kuwatambua wanahabari kama wadau muhimu wa kupewa mafunzo matokeo ya sensa ya watu na makazi.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto