November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makatibu Wakuu wapongeza kasi ujenzi wa mradi Julius Nyerere.

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAKATIBU Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wameridhidhwa na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere MW2115 kutokana na kazi inayofanywa na Mkandarasi.

Wamesema hayo walipotembelea mradi Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere MW2115 na kujionea mitambo ya kusaga mawe na kutengeneza zege, handaki la kuchepusha maji na sehemu ya kuvunia maji (power intake) katika mradi huo.

Katika hatua nyingine Makatibu Wakuu wameliipongeza Shirika la Umeme (TANESCO) kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, ambapo kukamilika kwake kutawasaidia Watanzania kukuza uchumi kwa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo ambayo vinahitaji nishati ya umeme.

Wakiongea katika ziara hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki, wamesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia wizara zao kuimarisha mambo mbalimbali hivyo wameiomba TANESCO kuendelea kumsimamia vizuri mkandarasi kama wafanyavyofanya sasa.

Awali akitoa taarifa katika ziara hiyo Mhandisi Mkazi wa Mradi, Mushubila Kamuhabwa amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 86 ya mpango kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dk Tito Mwinuka amewahakikishia Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Watanzania kwa ujumla kuwa mradi unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi amesema serikali itaendelea kutekeleza mradi huo kama walivyokubalina na mkandarasi na kwamba hadi sasa wametoa zaidi ya Shilingi trilioni moja kwa ajili ya mradi huo ambao utagharimu Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake Juni 2022.