Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,OnlineMwanza
SERIKALI imewataka makandarasi nchini kuacha ubinafsi na kuungana ili wapate nguvu ya mitaji na ujuzi wa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi yenye thamani kubwa.
Hayo yamesemwa jana jijini Mwanza na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano baina ya Bodi ya Makandarasi (CRB) na makandarasi mbalimbali wa kanda ya ziwa.
Alisema Serikali itafurahi kuona uwezo wa makandarasi wazalendo ukiimarika kwani wataweza kushindana na makandarasi wageni hivyo kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na fedha nyingi kubaki nchini kufanya kazi zingine.
“Acheni ubinafsi mfanye kazi kwa ubia, mkiungana ndipo mtapata uwezo wa kimitambo na utaalamu wa kushindanaa na wenzetu wa nje kwasababu hata hao wa nje mnaona wanafanyakazi kubwa kubwa hawako mmoja mmoja wengi ni kwasababu wameungana na kupata nguvu” alisema Waziri Chamuriho
Vile vile, aliwataka makandarasi kutaja majina ya maaofisa wa serikali wanaowaomba rushwa ili wapate zabuni za miradi ya ujenzi ili wachukuliwe hatua kali.
Waziri amesema uzoefu umeonesha kuwa mkandarasi anapopewa zabuni kwa rushwa anashindwa kukamilisha mradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana kutokomeza vitendo hivyo.
“Tupeni taarifa za watumishi wanaowaomba rushwa na sisi tutawalinda kwasababu tunajua mnashindwa kuwataja kwa kuhofia kwamba mtakosa zabuni zinazokuja. Rushwa inaleta athari kubwa sana kwenye hii kwa hiyo tunapaswa kushirikiana kwa karibu,” amesema
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Consolatha Ngimbwa amemshukuru Waziri akisema makandarasi wa imani kubwa kwamba kuwepo kwake kwenye wizara hiyo kutaleta ustawi kwao na kupiga hatua katika shughuli za sekta nzima ya ujenzi.
“Sisi makandarasi tunaimani kubwa na wewe na tunakuombea sana ili uweze kutimiza majukumu yako kwa ufanisi zaidi maana umekuwa bega kwa bega nasisi licha ya kuwa na majukumu mengi ofisini kwako,” alisema
“Naomba nikukumbushe tumekaa hapa tunasubiri ahadi yako uliyotoa kule Mbeya kwamba utatoa tamko kuhusu matumizi ya force account, mwaka 2018 serikali ilisema iliamua kutumia utaratibu huo baada ya kuona bei zetu ziko juu sana lakini sasa tumeshatoa mafunzo na tuko tayari kufanya kazi na serikali kwa bei ndogo,” alisema
Amesema CRB iliamua kuanza kutoa mafunzo maalum kwa makandarasi kwaajili ya kujaza zabuni tangu mwaka 2018 wamekuwa wakiwapa kozi hizo kwenye mikoa ya Morogoro, Arusha, Njombe, Dar es Salaam, Bukoba, Mwanza kwaajili ya kuwatayarisha makandarasi waingie kwenye ushindani miradi ya serikali.
“Makandarasi walishiriki mafunzo kwa wingi na kwa uhakika wako tayari kufanya hizo kazi na mfano mzuri ni jengo letu la Dodoma wakati ule linawekewa jiwe la msingi, Rais wa awamu ya tano hayati John Joseph Magufuli alifurahishwa na bei ambazo makandarasi wetu walitoa na alitaka tuendelee kutoa bei nafuu” amesema
More Stories
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima
Dkt.Biteko aagiza Kituo cha huduma kwa wateja Tanesco kusukwa upya
Rais Samia aridhishwa na uongozi safi wa Mwinyi