Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Leo Jumatano Agosti 21, 2024, ameshiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Mashindano ya Resi za Baiskeli, ambazo ni Sehemu ya Shamra-Shamra za Tamasha la Kizimkazi, huko Viwanja vya Koba Makunduchi, Mkoa wa Kusini, Unguja.
Hafla hiyo imeandaliwa kwa Mashirikiano ya Kamati ya Tamasha la Kizimkazi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, pamoja na Ofisi ya Rais Muungano, chini ya Udhamini wa Taasisi na Mashirika mbali mbali ikiwemo Benki ya Azania, TCB, NCAA, TANAPA, TPB na Chuo Kikuu cha Iringa.
Akitoa salamu zake mbele ya Hafla hiyo, Mheshimiwa Othman amehimiza wajibu wa Serikali katika kuendeleza urithi wa alama za utambulisho wa jamii, kwaajili ya maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema maendeleo na uchumi wa Nchi yoyote, hutegemea kwa kiasi kikubwa urithi na alama za utambulisho wa jamii, ambazo pia ni kivutio kikubwa katika kukuza Sekta ya Utalii, ambayo ni njia yenye umuhimu wa pekee wa kukuza pato la Taifa.
Hivyo Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa miongoni mwa namna bora ya kuendeleza urithi wa alama muhimu zinazoitambulisha Jamii na Nchi kwa ujumla ni kupitia Matamasha, likiwemo Tamasha la Kizimkazi.
Aidha, Mheshimiwa Othman ameshukuru Hatua za Makusudi zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan; na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuliungamkono Tamasha la Kizimkazi, ambalo ni muhimu kwa kukuza Uchumi wa Nchi, kupitia Sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Othman akikumbusha miongoni mwa Alama hizo ambazo zimeanza kufifia, ametaja Tawala za Asili hapa Visiwani, Ukiwemo Utawala wa Malkia Fatima wa Kizimkazi, Karne kadhaa zilizopita, ameshauri Waandalizi wa Matamasha kuzingatia Weledi katika Lugha, na ikibidi iwepo Siku Maalum ya Wamalenga hapa Nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema Dhamira ya Shamra-Shamra zote hizo ni kuyagusa moja-kwa-moja maisha ya kawaida ya mwananchi katika kuyafikia maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrik Soraga ambaye amehamasisha kikamilifu uelewa na ushiriki wa vijana wa Zanzibar amesema, Tamasha la Kizimkazi ni Eneo Muhimu la Kuzalisha fursa za Maendeleo ya Uchumi wa Nchi, hasa kupitia Sera na Sekta za Utalii Endelevu.
Akiwasalimia washiriki wa Hafla hiyo pamoja na Wanamichezo, Mwenyekiti wa Tamasha la Kizimkazi, Mwalimu Mahafoudh Said Omar, ameshukuru na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Viongozi wa Serikali, Mamlaka, Taasisi, Jumuiya na Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia katika kuungamkono harakati za maendeleo katika Jamii, huku akiwaasa Wananchi wasivunjike moyo kufanikisha ndoto zao, ili kujikwamua kiuchumi na kimaisha kwa ujumla.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, Mawaziri, Vyama vya Siasa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa Makampuni na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, pamoja na Wananchi, wamehudhuria katika hafla hiyo, wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman.
Shamra-Shamra hizo zimehusisha harakati mbali mbali, zikianza na Fainali za Michezo ya Kabadi, Mpira wa Wavu, Mbio za Baiskeli kwaajili ya Wenyeji na Watu wenye Ulemavu, pamoja na Mashindano kwaajili ya Waendesha-Baiskeli, kuanzia Mjini hadi Koba Makunduchi na Maelezo Mafupi juu ya Mtazamo wa Tamasha la Kizimkazi.
Awali, Mheshimiwa Othman amepokea Resi za Baiskeli kwa wachezaji maalum ambapo washindi ni (1) Hassan Khamis Tajo, (2) Kheri Joba Juma na wa (3) ni Ahmed Simai Tajo.
More Stories
Samia atua Kariakoo, ashuhudia yaliyojiri
Lugangira:Tunapambania mitaa 28
Waziri Mavunde awakaribisha wawekezaji wa madini kutoka Finland