December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla,azindua kampeni Serikali za Mitaa Dar

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA.Amos Makalla,Novemba 20,2024,amezindua rasmi kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Dar-es-Salam katika viwanja vya Buliaga vilivyopo Kata ya Miburani, Wilaya ya Temeke mkoani hapa.

CPA.Makalla akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Temeke,amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM),kina kila sababu ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo, kwani kimefanya maandalizi ya kutosha ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya chama,2020/2025 kwa asilimia kubwa.

Pia amewataka wananchi hususani wanachama wa CCM kuwachagua wagombea wa chama hicho,waliopewa dhamana ya kugombea nafasi katika uchaguzi huo,kwani kimesimamisha wenye vigezo na sifa za kuwatumikia wananchi katika maeneo yao.

Pia, amesema kuwa, zipo sababu mbalimbali za kukipa ushindi chama hicho, huku akisema ndiyo chama chenye dhamana ya kuwahudumia wananchi wake ikiwa pamoja na kuwaletea maendeleo mbalimbali.

“CCM itashinda kwa kishindo,tumezindua kampeni nchi nzima,tutafanya kampeni za uhakika na za kistaarabu, bila lugha chafu,tumewateua wagombea wazuri na tutawaonesha Watanzania kuwa ni chama Cha kistaarabu na kiongozi,”amesema.

Amesema wanazo hoja za kutosha hivyo watazitumia kunadi wagombea, kuhakikisha wanawashawishi wananchi kuwachagua.

“CCM itashinda kwa kishindo kwa kupigiwa kura, tunaomba msibweteke mkajua CCM itashinda tu, hapana mjitokeze mkapige kura Novemba 27,2024,”.

Hata hivyo amesema,lengo la CCM ni kushika dola, hivyo wamejipanga kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ndiyo msingi wa ushindi wa kishindo kwa Uchaguzi Mkuu.