January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla ammwagia sifa Rais Samia uwekezaji DPW Bandari Dar

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline. Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mfunzo wa CCM, Taifa, CPA Amos Makalla, amepongeza juhudi zilizofanywa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uboreshwaji mkubwa uliofanywa katika Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA).

CPA Makalla akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali leo Agosti 28, 2024 Jijini Dar es Salaam, ametoa pongezi hizo kwa Rais Samia, baada ya kupokea wasilisho la utendaji wa bandari ya Dar es Salaam baada ya kufanyika kwa uwekezaji wa DPW.

Amesema ni vyema wananchi wakaelewa na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi, huku akidai kuwa, uboreshwaji wa bandari ya Dar es Salaam uliofanywa na muwekezaji DPW ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi.

“Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mimi kama Mwenezi tunatoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyofanya katika kuboresha bandari hii kwa kuongeza nguvu na kumpa muwekezaji DPW.

Kupinga na kupanga ni wajibu wa watu na CCM ni chama cha kupanga na kuwaletea wananchi maendeleo na itaendelea kuwaletea wananchi maendeleo kama haya na asiyeona maendeleo katika bandari hii huyo hajawahu kufika Dar es Salaam tangu azaliwe ndo mara yake ya kwanza au hana akili timamu!

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu TPA, Juma Kijavara amesema Kampuni ya DPW imewekeza Dola Milioni 250 sawa na Sh. Bil 275 kiasi ambacho tayari kimewekeza katika ununuzi wa mitambo ya kisasa, urekebishaji wa mitambo iliyokuwa ya TPA na usanifu na usimamizi wa mfumo wa TEHAMA.

Pia amesema, kufuatia kuingia kwa muwekezaji huyo DPW kumeongeza thamani ya bandari hiyo bila ya kuathiri ajira za wafanyakazi wa TPA na kusema kuwa, takribani ya zaidi ya wafanyakazi 350 wamehamishwa DPW na hakuna wafanyakazi walioachishwa kazi.