Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, amesema wanamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni yake ya kuitangaza Tanzania kwa kuendelea kuliweka safi jiji hilo ili kuvutia watalii na wawekezaji.
Akizungumza jana wakati wa usafi wa Jumamosi ya mwisho wa mwezi uliofanyika kuanzia makutano ya taa za Buguruni hadi nje ya kiwanda cha Bakhresa Tazara, alisema kampeni ya safisha Pendezesha Dar es Salaam tayari imeanza kuleta mafanikio.
“Mheshimiwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuitangaza Tanzania nje ya nchi, amezindua filamu ya Royal Tour maana yake anawaita wawekezaji, watalii, wadau mbalimbali wa maendeleo, wapo watakaopitia KIA na wengine Dar es Salaam, kama tusingefanya maandalizi ya kuwapanga vizuri wamachinga, kuwa na kampeni endelevu ya usafi ingekuwa kazi bure.
“Sasa hivi tunao uwezo wa kutembea kifua mbele waje kwa sababu Dar es Salaam ni safi na wakija wengi ndipo tunapopata riziki, zamani ukitoka Airport mpaka unakaribia Ikulu ni mabanda kulia, kushoto…sasa mtalii gani atakuwa ku -enjoy hapa,”? alihoji Makala.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, alisema eneo hilo linaloanzia kwenye taa za Buguruni hadi pembenzoni mwa Kiwanda cha Bakhresa ni korofi kutokana na baaadhi ya wafanyabiashara walioondolewa kurudi tena na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
“Kuna vurugu zimetokea kama mara mbili na wakati mwingine wanakuwepo vijana wakorofi ambao wanawahamasisha wenzao na kuanza kurusha mawe, alisema Ludigija.
Mkuu huyo wa mkoa pia alipokea mapipa 20 ya kuhifadhia taka na na mafagio yaliyotolewa na wadau mbalimbali kupitia uratibu uliofanywa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Tawi la China na kukabidhiwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam Mussa Kilakala .
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora