December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ismail Aden Rage.

Makada 22 CCM wajitosa Tabora Mjini, yumo Ismail Aden Rage

Na Allan Vicent, Tabora

ZOEZI la uchukuaji fomu za kugombea ubunge na udiwani kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Tabora mjini limeanza kwa kasi kubwa ambapo wana-CCM wapatao 22 wamejitokeza siku ya kwanza kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo la Tabora mjini akiwemo kada Ismail Aden Rage.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Katibu wa CCM wilaya ya Tabora mjini, Vailet Kasanga amesema kuwa mwaka huu kuna mwitikio mkubwa sana wa wananchi kugombea nafasi za ubunge na udiwani tofauti na uchaguzi uliopita.

Amesema kuwa katika siku ya kwanza tu (jana) waomba kugombea ubunge waliochukua na kurudisha fomu zao ni Emanuel Mwakasaka, Kasya Adam Kasya na Costantine Manda, huku wengine walichukua fomu wakiwa ni wakili wa kujitengemea Emanuel Musyani .

Ametaja wengine waliojitokeza kuwania ubunge kuwa ni wanawake wawili ambao ni Halima Mnenge na Zainab Kifu wakiwemo Shekhe Sharif Mikidadi na Ismail Aden Rage.

Wengine kuwa ni James Isakari, Stephine Warioba, Mbela Kaluzi, Ngasa Mangombe, Saidi Makaranga na Godbless Mafore.

Amesema kwamba wengine ni Prof Fadhili Mgumia ,Dkt Deusdedi Kanuni, Emanuel Manzilili, Othumani Kipeta, Kisamba Tambwe ,Joseph Gimbuya, Amani Muhamed na Dickson Leonard.

Aidha Kaimu Katibu wa Umoja wa Wanawake wilayani humo, Frola Nyakasi amesema kuwa wanawake waliojitokeza kuchukua fomu za udiwani viti maalum kwa siku ya kwanza tu idadi yao imefikia watu 34.

Amebainisha kuwa wanawake hasa kundi la vijana wamehamasika sana kugombea nafasi za udiwani viti maalum kuliko kundi la kinamama wazee.

Naye Katibu Kata wa CCM kata ya Kidogochekundu, Abdallah Mfaume amesema kuwa watu waliojitokeza siku ya 1 kuchukua fomu ya udiwani wa kata hiyo wamefikia 10.

Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Emanuel Mwakasaka baada ya kurudisha fomu ya ubunge amesema kuwa amegombea tena ili kumaliza kazi za wananchi alizozianzisha.

Amewataka wanachama wa chama hicho kumchangua tena ili kuendeleza mazuri aliyoanzisha na kuyakamilisha katika awamu hii 2020-2025 hasa umeme wa REA na miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mvua za masika mwaka huu.