April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majiko ya umeme mbolea mpya kwa maendeleo, uhifadhi mazingira

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ametoa wito kwa wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla, kuhamasika na kuanza kutumia majiko ya umeme kwa ajili ya kupikia, akibainisha kuwa teknolojia hiyo ni rafiki wa mazingira na gharama zake ni nafuu ikilinganishwa na nishati nyingine za kupikia.

Akizungumza baada ya kukagua banda la majiko ya nishati safi ya umeme katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Kiongozi huyo amesema matumizi ya majiko hayo yatasaidia pia katika kutunza mazingira, kupunguza ukataji wa miti, na kuongeza pato la taifa.

“Muda umefika sasa kwa Wananchi wa Bagamoyo kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Aidha, amefafanua kuwa majiko ya umeme ni fursa adhimu kwa Watanzania kwa kuwa matumizi yake ni ya gharama nafuu zaidi, ambapo mtumiaji anaweza kupika aina mbalimbali za vyakula kwa muda wa saa moja kwa kutumia wastani wa unit moja ya umeme inayogharimu shilingi 350 tu.

Kwa mujibu wa Kiongozi huyo, matumizi ya majiko haya yatapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa kuni, mkaa na mafuta ya kupikia, hivyo kusaidia kuokoa mazingira na kupunguza madhara ya kiafya yatokanayo na moshi.

Mwenge wa Uhuru umeendelea kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kote nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi.