Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
SHULE ya msingi Majeleko iliyopo katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ni miongoni mwa shule ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya madawati,uhaba wa walimu,matundu ya vyoo na vitendea kazi vya walimu kama kompyuta na Printa.
Pia mtandao huu ulijionea changamoto ya uchakavu wa majengo (vyumba vya madarasa) hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi kwa hofu ya majengo hayo kuweza kuanguka wakati wowote lakini hata yaliyo mazima hayana milango,hayana madirisha wala hayajasakafiwa ilhali wanafunzi wanakaa chini kutokana na upungufu wa madawati uliopo shuleni hapo.
Licha ya mafanikio ya kitaaluma katika shule hiyo ,lakini inawezekana kupitia changamoto hizo walimu wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwamba kama mazingira yangekuwa mazuri shule hiyo huenda ingeweza kufanya vizuri zaidi.
Hali ya changamoto hizo unakisukuma Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) kupitia Umoja wa Wanawake wa Chuo hicho (UWAMI) kutoa msaada wa madawati 25 yenye zaidi ya thamani ya shilingi milioni 3.0 ili kukabili changamoto ya madawati na hivyo kufanya shule hiyo kuwa na madawati 94.
Magina Magendo ni mwalimu katika shule hiyo ambaye alisoma risala ya shule mbele ya Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mipango kwa niaba ya Mkuu wa shule hiyo Maulida Semniga ambapo anaelezea mafanikio pamoja na changamoto zinazoikabili shule hiyo ambapo anasema….
“Shule ya Msingi Majeleko inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati ,uchakavu wa miundombinu hasa vyumba vya madarasa ,matundu ya vyoo na upungufu wa walimu.”
Mwalimu Magendo anasema,shule hiyo ambayo imeanzishwa mwaka 1953 ,ina jumla ya wanafunzi 581 wakiwemo wanafunzi wa elimu ya awali 74,walimu saba,vyumba vya madarasa vinane ,madawati 69 na matundu ya vyoo yapatayo sita.
“Tangu kuanzishwa kwa shule hii yapo mafanikio lakini pia zipo changamoto zinazoikabili shule hii ikiwemo upungufu wa walimu,madawati,uchakavu wa miundombinu pamoja na ukosefu wa vitendea kazi kama mashine ya photocopy kompyuta na printa .”anasema Mwalimu Magendo.
Hata hivyo anasema uongozi wa shule kwa kushirikiana na wananchi wanafanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuchangishana michango ya kila kaya kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya shule hiyo ambapo anasema lengo ni kukusanya shilingi milioni 5.3 na kwamba mpaka sasa wameshakusanya shilingi milioni 2.8.
Aidha anaiomba Serikali kupitia wilaya ya Chamwino kusaidia katika kutatua changamoto hizo ili kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kuchangia maendeleo mazuri hasa katika madarasa ya mitihani.
Hali ya ufaulu wa matokeo ya darasa la saba katika shule ya Msingi Majeleko umekuwa ukishuka kutoka asilimia 96 mwaka 2018hadi kufikia asilimia 79 mwaka 2021.
Changamoto darasa la elimu ya awali zaelezwa
Magdalena Damian ni mwalimu wa darasa la elimu ya awali katika shule ya msingi Majeleko ambaye anazungumiza hali ya uchakavu wa majengo hususan wa darasa la elimu ya awali ambapo anasema hali jengo hilo ni mbaya na wakati mwingine inamlazimu kuwafundishia watoto nje ili kuwanusuru na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa masomo na kuathiri afya zao.
Vile vile anazungumzia changamoto ya uhaba wa walimu wa darasa la awali na darasa la kwanza huku akisema kwanza darasa la awali ni dogo inamlazimu kufundisha kwa awamu ambapo wapo wanaoingia saa mbili na kutoka saa tano asubuhi na wengine kuanzia saa tano mpaka saa tisa alasiri lakini hapo hapo bado inamlazimu kufundisha na darasa la kwanza.
“Tunaiomba Serikali iliangalie hili,darasa ka kwanza linatakiwa liwe na mwalimu wake na darasa la kwanza liwe na mwalimu wake ili tuweze kufanya kazi ya kufundisha watoto hawa kwa ufasaha zaidi kwani ndio kipindi ambacho tuajenga msingi wa ujifunzaji wao.”anasema mwalimu huyo
Kauli ya Serikali
Hata hivyo Afisa Elimu Michezo wa Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Nicholaus Achimpota ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Chamwino Gift Msuya katika hafla hiyo ya kukabidhi madawati hayo anawataka wananchi wa kijiji hicho kuanza ujenzi angalau ufikie kwenye lenta ndipo Serikali nayo iweze kuwasaidia ujenzi kwa kumalizia maboma hayo.
“Mnapojenga jengo lenu mkafikia ngazi ya lenta serikali inamaliza lote pamoja na kuweka madawati ,sasa kama hakuna kilichowekwa serikali itawasaidiaje,leo tuna maboma ambayo yanatakiwa kumaliziwa kwenye kata na shule mbalimbali katika wilaya yetu ya Chamwino,
“Hapa tumepita kuona majengo yenu na tumeona kweli yanahitaji ukarabati je ninyi mmeonyesha nini,shika ili ushikamane,sasa wananchi wa Majeleko tuonyeshe kwa sababu siyo lazima kutoa pesa hata nguvu kazi ,tuanze kuonyesha juhudi kuwa na sisi tuna jambo.”anasema Kaimu Mkuu huyo wa wilaya.
Ashtukia mwenendo wa ukusanyaji michango
Katika hotuba yake ,Achimpota alihoji sababu za wananchi kutoendelea kutoa michango hiyo ya uboreshaji miundombinu ya shule ikiwemo majengo.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Vedastus Timothy anasema tukio hilo ni kuonyesha watoto wa shule ya Majeleko ni kama watoto wengine wanaohitaji miundombinu mizuri ya shule ili wasome katika mazingira mazuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAMI ambaye pia ni Mwanasheria wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Aisha Mjegele anasema wameamua kutoa madawati kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya wananwae Duniani ambayo hufanyika Machi 8 ya kila mwaka huku akizitasa taasisi nyingine ,wazazi pamoja na wadau wa elimu kushiriki kikamilifu katika kujitoa kusaidia miundombinu ya shule mbalimbali ili watoto wasome katika mazingira bora.
Wanafunzi wazungumza
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao,wanafunzi Gloria Mfugwa na Zawadi Malima wamekishukuru Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini kwa msaada wa madawati 25 huku wakisema bado kuna changamoto nyingine nyingi zinazo ikabili shule hiyo ikiwemo uchgakavu wa madawati.
“Tunashukuru kwa msaada wa madawati lakini bado tuna uhitaji wa madawati maana pamoja na haya tuliyopewa lakini bado madawati ni machache,watoto tunanyanyasika tunanyang’anyana madawati,wengine wanachafuka kutokana na kukaa chini ,lakini pia shule yetu ina uchakavu wa madarasa.” Anasema Glory
Kwa upande wake Zawadi ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba anasema tangu alipoanza darasa la kwanza ameekuta shule hiyo ina uhaba wa madawati na uchakavu wa majengo .
“Wanafunzi wengi hapa wanakaa chini ,mfano kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la nne hakuna madawati,wanafunzi wengine wanatoroka shule kwa sababu ya kukaa chini.”anasema Zawadi.
Viongozi wa vitongoji waeleza sababu za michango kusimama
Kwa upande wao viongozi wa vitongoji katika kijiji cha Majeleko wanasema michango hiyo imesimama kutokana na wananchi kuwa na hofu ya pesa zao kutofanya kazi iliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwongozo ambacho shule ya Msingi Majeleko ipo David Haroun anasema viongozi wa vitongoji walipewa kazi ya kuchangisha na wamefanya hiyo ingawa kuna baadhi ya wananchi bado hawajachangia.
Anasema,wananchi ambao bado hawajachangia wana hofu na pesa zao kuliwa kwani wananchi walishaomba fedha zilizotolewa zianze kufanya kazi ili kuhamasisha ambao hawajachanga wafanye hivyo lakini hakuna kinachoendelea.
“Shule hii ipo katika kitongoji changu cha Mwongozo na mimi ndio mwenyekiti wa kitongoji hiki,kimsingi marasa ni mabovu yanaweza kuangukia wanafunzi ,vyoo vya wananfunzi wa kiume ni changamoto ,
“Kwa mfano Darasa hili la elimu ya awali ni la zamani mimi tangu nimeanza shule mwaka 1982 nimelikuta na limejengwa kwa tope,tunaiomba Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Chamwino itusaidie kujenga vyumba vya madarasa kwani watoto wanateseka.”anasema Haroun
Anasema pesa za awali ambazo zimechangwa na wananchi wamekabidhi kwa mtendaji wa kijiji hicho lakini wananchi wanashangaa kwa nini ujenzi huo hauanzi.
Wananchi ambao bado hawajachangia wapo tayari kufanya hivyo ,lakini wanataka mpaka hizo pesa zianze kufanya kazi ndipo na wao waendelee kuchangia .
Kwa upande wake Elizabeth Muhila anasema,wanafunzi wengi bado wanakaa chini kutkana na ukosefu wa madawati .
“Kwa mfano ukiingia darasa la tatu kuna adawati moja tu ambalo wanakaa wanafunzi watatu hadi wanee na wanaosalia wote wanakaa chini.”anasema Muhila
Baadhi ya wazazi ambao hawakutaka kutaja majina yao wanasema kuwa wananchi wengi wanachotaka kuona kazi imeanza ndipo waendelee kuchangia pesa kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule yakiwemo majengo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam