January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:The Great Ruaha Marathon ina maslahi mapana kwa Taifa

Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Ruaha

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa (Mb) amesema mbio za The Great Marathon zilizofanyika leo tarehe 06-07-2024 ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha zina maslahi mapana kwa Taifa kutokana na unyeti wake wa kukuza utalii Nyanda za juu Kusini.

Akiwa katika eneo la Ibuguziwa kando ya mto The Great Ruaha Majaliwa alisema hizo ni mbio pekee katika Mikoa ya Kusini zinazokimbiwa ndani ya hifadhi zikibeba dhima nzima ya kuutangaza utalii ili taifa liendelee kupata mapato yatokanayo na ujio wa watalii wa ndani na nje.

Aidha,Majaliwa aliongeza, mbali na utalii mbio hizi pia zimelenga kujenga uelewa kwa wananchi kulinda na kuhifadhi vyanzo vya mto The Great Ruaha ili uendelee kuimarisha ikolojia ya hifadhi yetu na kuchangia uzalishali wa maji yanayoenda katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Nyerere ili kupata nishati ya umeme ya uhakika nchini.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula (Mb) akimkaribisha Waziri Mkuu alisema wameshiriki mbio hizo kwa mara ya tatu mfululizo huku hamasa na idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka, kuongezeka kwa washiriki kuna mchango katika idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hii na kuongeza kipato kwa jamii zinazokaa kandokando kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa wanamichezo hao.

“Mbio hizi zimeandaliwa kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Kusini mwa Tanzania, Hifadhi ya Taifa Ruaha ikipewa kipaumbele kulingana na baioanuai zilizomo. Hifadhi hii imejaliwa kuwa na wanyamapori anuai na mandhari nzuri ambazo zimeendelea kuvuta watalii wengi, na hili limedhihirika baada ya kila mwaka idadi ya watalii imeendelea kuongezeka,”alisema Kitandula.

Awali, akiukaribisha ugeni huo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana Mwishawa alisema, “TANAPA itaendelea kuhifadhi mto The Great Ruaha kwani ndio kitovu cha Uhifadhi na Ikolojia ya hifadhi hii.

“Zaidi ya kilometa 160 za mto huu hupita ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa mantiki hiyo utaona ni jinsi gani ulivyo muhimu kwa Ikolojia ya hifadhi hii, hivyo tukuhakikishie Waziri Mkuu, tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaokaa katika vyanzo vyake wasiharibu vyanzo hivyo ili mto huu uendelee kutiririsha maji kwa mustakabali wa hifadhi hii na Taifa kwa ujumla”, aliongeza Kamishna Mwishawa.

Mbio hizo za The Great Ruaha Marathon zilizofanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha zimeshirikisha wanamichezo 630 zikihusisha Mbio za kilometa 5, 10, 21 na 42. Viongozi wengine walioambatana na Waziri Mkuu ni pamoja Mhe. Peter Selukamba Mkuu wa Mkoa Iringa, Wabunge wa Mkoa wa Iringa, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Iringa pamoja na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali.