December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Urithi wa ukombozi Afrika ni lulu kwa Watanzania

Na Jovina Bujulu,TimesMajira online, MAELEZO

HIVI karibuni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika iliandaa kongamano la kuenzi mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika likiwa na lengo la kutambua, kuuenzi na kujivunia historia tukufu ya nchi yetu pamoja na mchango wa Tanzania katika kufanikisha harakati za ukombozi wa nchi za Afrika.

Akihutubia katika kongamano hilo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anasema kuwa kongamano hilo linawalejesha Watanzania katika mshikamano, umoja, uzalendo, na utaifa uliojengwa katika kuhakikisha wenzetu wa Afrika wanakuwa huru.

“Urithi huu wa ukombozi uliopo nchini ni lulu kwetu, na kwa sasa jukumu letu ni kuutumia kujikomboa kiuchumi na kifikra, hivyo ni vema jamii ambazo zinatumia au zinamiliki maeneo au miundombinu ya urithi wa ukombozi wa Afrika ikavitunza na kupata ushauri wa kitaalamu kuanzisha makumbusho na kuvutia utalii katika eneo hilo ili kujiongezea kipato”, anasema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia umuhimu wa ukombozi , Waziri Mkuu Majaliwa alinukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema kuwa “ Hatuwezi kusema kuwa Tanzania tupo huru, wakati nchi nyingine za Afrika hazipo huru”. Maneno hayo yalikuwa na lengo la kusisitiza kuzidisha mapambano ya kuzikomboa nchi zote za Afrika ili bara zima la Afrika liweze kusema na kujivunia uhuru.

Waziri Mkuu Majaliwa anaitaja mikoa ya Lindi, Songea, Mtwara, na Mbeya kuwa anatarajia iwe ya kwanza kunufaika na zao jipya la utalii wa kiukombozi na kubainisha kuwa kuna maeneo zaidi ya 225 ya urithi wa ukombozi nchini ambayo mengi yapo katika mikoa hiyo ya Kusini mwa Tanzania. Historia ya nchi inaonesha kuwa mikoa hiyo ilitumiwa sana na wapigania uhuru waliokuwa wanatoka nchi za Kusini mwa Afrika na kuweka kambi katika mikoa hiyo.

Aidha, anasema kuwa harakati za ukombozi wa Afrika zilihusisha makundi mbalimbali katika jamii kama vile kundi la wanasiasa, dini, vyama vya ushirika, wanamuziki, wanamichezo, wasanii, machifu, wazee wa kimila, wasomi na makundi mbalimbali ya haki za binadamu pamoja na taasisi za kimataifa. “ Ndani ya makundi haya yote upo urithi ulioachwa ambao sisi kama wahusika yatupasa kuulinda ili kizazi kijacho kijifunze na kuuendeleza”, aliongeza Majaliwa.

Anatoa wito kwa Watanzania wote au mtu yoyote ambaye ana amali za urithi wa ukombozi kuzipeleka katika Makumbusho ya ukombozi wa Afrika iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Ninaposema amali namaanisha urithi unaoshikika au usioshikika iwe chombo, iwe muziki, iwe nguo, au aina yoyote ya kitu kilichotumika wakati wa harakati za ukombozi na chenye uhalisia wa kihistoria au simulizi zake, naomba mtu , kundi au taasisi hiyo kama itaridhia iviwasilishe katika Makumbusho ya urithi wa ukombozi wa Afrika iliyopo Dar es Salaam, mtaa wa Garden Avenue, mkabala na Ubalozi wa Kanada tuvipeleke vitu hivyo ili vihifadhiwe kitaalamu visije vikapotea”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia namna ya kuenzi na kujivunia historia ya ukombozi, Majaliwa anawataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii huku wakilinda wasilimali zetu kwa uzalendo, kuendelea kuwa na utangamano, utaifa na uzalendo kwa kuenzi mazuri yaliyoachwa na wapigania uhuru wa nchi yetu pamoja na kuitangaza nchi yetu kwa mazuri yanayoendelea kufanyika ili kuvutia wawekezaji katika sekta zote nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa aliyataka makundi mbalimbali yaliyoshirikishwa katika Kongamano hilo kwa kutambua nafasi zao katika jamii na mchango walioutoa katika kuhakikisha Bara la Afrika linakuwa huru kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu kuenzi historia ya ukombozi iliyopo nchini.

Aidha, Bashungwa alisema Kongamano hilo lililenga kusherekea, kuenzi, kulinda, kutangaza na kuendeleza miundombinu na historia ya kipekee ya harakati za ukombozi wa Afrika iliyopo nchini, pamoja na kuelimisha umma umuhimu wa kujikomboa kiuchumi, na kifikra kupitia uhifadhi na utangazaji wa zao la utalii wa kiukombozi na kuhamasisha jamii kuwa na utangamano wa kitaifa ambao huzaa uzalendo, mshikamano na upendo.

“Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2011 ya kuwa Tanzania iwe Mako Makuu ya Uhifadhi wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ili urithi huo usipotee kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo”, alisema Bashungwa.

Kongamano hilo lililofanyika jijini Dar es Salaam liliwashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya Urithi wa Ukombozi wakiwemo machifu na wazee wa kimila, maafisa Utamaduni na Michezo, wakuu wa Vyuo na Shule za Msingi, wanafunzi wa Vyuo na Shule za Msingi pamoja na Wasanii.

Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika ilianzishwa nchini Tanzania mwaka 2011 baada ya kuridhiwa na Mkutano wa 16 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kupitia Azimio namba 357. Majukumu ya Programu hii ni pamoja na kutambua , kuhifadhi, kulinda, kuenzi, kuendeleza na kutangaza Urithi wa Ukombozi wa Afrika ikiwa ni pamoja na kuratibu tafiti na kutangaza taarifa za Urithi wa Ukombozi wa Afrika kwa kushirikiana na wadau na wanataaluma.

Aidha, Programu hii ina jukumu la kuendeleza utalii wa kiukombozi nchini kwa kushirikiana na wadau na mamlaka yenye dhamana ya utalii pamoja na kuendeleza ushirikiano baina ya nchi wanachama wa Programu katika kusimamia na kuendeleza Urithi na Ukombozi wa Afrika.