Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametoa agizo kwa Wizara ya Kilimo kuhakikisha inakuza matumizi ya teknolojia za kisasa za umwagiliaji nchini kwa kushirikiana na sekta nyingine za umma pamoja na sekta binafsi.

Akizungumza katika maonesho ya wakulima ya Nane Nane 2025 yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Majaliwa alisisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Wizara ya Kilimo ina jukumu la msingi la kushirikisha wadau wote kuimarisha mifumo ya kisasa ya umwagiliaji ili kuongeza tija katika kilimo.
“Natoa agizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Gerald Mweli, kuhakikisha kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inashirikiana na taasisi nyingine za serikali na sekta binafsi kuvutia uwekezaji wa mitambo na teknolojia za kisasa za umwagiliaji nchini,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika ziara yake kwenye kijiji cha mitambo ya umwagiliaji kilichopo ndani ya viwanja vya maonesho, Majaliwa alipongeza juhudi za Tume ya Umwagiliaji kwa kuonyesha mifumo ya kisasa kama center pivot, ambayo ina uwezo wa kumwagilia hadi hekta tano (sawa na ekari 12.5) ndani ya saa 24. Mtambo huo unaambatana na teknolojia za kutambua unyevu wa ardhi, kuweka mbolea kiotomatiki, na kutabiri hali ya hewa.

“Teknolojia hizi si kwa kilimo tu bali hata sekta nyingine kama michezo. Umwagiliaji mdogo unaweza kusaidia ujenzi wa viwanja vya michezo vyenye majani halisi. Mfano, uwanja wa Dodoma una ukame mwingi; tukipata mitambo hii, milango ya uwekezaji itafunguka zaidi,” alieleza Waziri Mkuu.
Aidha, alisisitiza kuwa taasisi kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Magereza, na wakulima wakubwa kama wale wa Iringa wanapaswa kuwezeshwa kupata mitambo hii ili taifa lijitosheleze kwa chakula.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Gerald Mweli, alisema kuwa wizara yake inashirikiana na uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuwawezesha vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia hizo mpya.



Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alisema kuwa Tume imejipanga kuendeleza elimu ya matumizi ya teknolojia za kisasa hata baada ya maonesho, kupitia kijiji cha mitambo kilichowekwa kudumu katika viwanja vya Nane Nane, Dodoma.
“Hii itakuwa ni fursa ya wakulima kujifunza kwa vitendo namna teknolojia hizi zinavyofanya kazi, pamoja na kuelewa namna serikali inavyowekeza katika kilimo cha umwagiliaji,” alisema Mndolwa.
Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Dodoma, Oswald Urasa, aliongeza kwa kuelezea uwezo wa mitambo hiyo ya kisasa, akisema kuwa uwepo wa mifumo jumuishi ya mbolea, hali ya hewa na unyevu wa ardhi kunarahisisha kazi ya wakulima na kuongeza uzalishaji kwa kiwango kikubwa.
Kwa ujumla, hatua hizi zinaakisi azma ya serikali kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mapinduzi ya kiteknolojia, huku lengo kuu likiwa ni kuongeza uzalishaji, kuhakikisha usalama wa chakula, na kukuza uchumi wa nchi kupitia kilimo endelevu cha umwagiliaji.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina