March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Taasisi Zote za Umma Zijiunge na GovESB Kabla ya Julai 30, 2025

Majaliwa: Taasisi Zote za Umma Zijiunge na GovESB Kabla ya Julai 30, 2025

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma 

WAZIRI  Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza taasisi zote za umma ambazo bado hazijajiunga na Mfumo wa Mawasiliano ya Kielektroni Serikalini (GovESB) kuhakikisha zinafanya hivyo kabla ya Julai 30, 2025 huku akiipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni mfumo huo .

Amesema lengo la taasisi zote za Umma kujiunga na mfumo huo ni kuhakikisha Serikali inatumia kikamilifu teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akihitimisha maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma katika viwanja vya Chinangali Park jijini  Dodoma,Waziri Mkuu Majaliwa amesema  hilo ni agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan lankutaka mifumo isomane ili Serikali iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Taasisi zote , hakikisheni mnakuwa sehemu ya GovESB,huu ni msisitizo kutoka kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwamba kila taasisi inapaswa kuwasilisha mfumo wake kwa eGA bila gharama wala uhitaji wa bajeti mpya ili mifumo yote ya Serikali iweze kusomana.” amesiditiza Majaliwa.

Waziri Mkuu pia alizihimiza taasisi zote za umma zinazomiliki au kubuni mifumo mipya kuhakikisha mifumo hiyo ina uwezo wa kuwasiliana na kubadilishana taarifa kupitia GovESB ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, ameiekeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha kuwa mifumo yote iliyounganishwa inabadilishana taarifa kikamilifu na kwa wakati.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alisema Tanzania imepata kutambuliwa kimataifa kutokana na hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ya Serikali Mtandao. Alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia mwaka 2022, Tanzania ilipanda daraja kutoka kundi B hadi A, na kushika nafasi ya 26 duniani, ya pili Afrika na ya kwanza Afrika Mashariki katika ukomavu wa huduma za kidijitali serikalini.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Ndomba amesema,Mamlaka hiyo Benedict Ndomba umefanikiwa kutekeleza agizo la Rais dkt.Samia  la kujenga na kusimamia mfumo wa ubadilishanaji taarifa serikalini (GovESB)

Katika tukio hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alizindua rasmi mifumo miwili mikuu ya GovESB ambao Mfumo wa kielektroni unaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa na mfumo wa e-Wekeza – Mfumo unaomwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza moja kwa moja katika Mfuko wa Faida .