February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa afunguka Rais Samia anavyochapa kazi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni tiba ya maendeleo, hivyo Watanzania wanapaswa kwenda naye, kwani ataifikisha nchi kule kunakotarajiwa.

Amesema Rais Dkt. Samia ni kiongozi anayeona, kusikiliza na kutatua changamoto za Watanzania kwa ustadi wa hali ya juu na amedhihirisha hilo katika kipindi chake cha uongozi.

Amesema hayo leo wakati Mkutano Mkuu Maalum Chama Cha Mapinduzi, Jimbo la Maswa Mashariki, uliofanyika katika uwanja wa nguzo nane,Maswa mkoani Simiyu.

“Rais Dkt. Samia kwa uwezo wake na maono yake ameonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania, wote tumeshuhudia nia yake ya kusimamia utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali za maendeleo na tumeona namna alivyosimamia na kukamilisha miradi yote ya kimkakati,” amesema Majaliwa.

Akizungumzia sekta ya maji, Majaliwa amesema kuwa Serikali ya CCM imedhamiria kuhakikisha inatekeleza miradi mikubwa ya maji kutoka katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji safi na Salama.

“Mpango wetu ni kuendelea kufikisha huduma ya maji mpaka vitongojini,” amesema.

Kadhalika, Majaliwa amesema kuwa katika sekta ya afya Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa na kuwapunguzia adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa Umeme inaimarika nchini, Serikali imeendelea kutekeleza miradi umeme.

“Tumeshafikisha umeme karibu asilimia 99 kwenye vijiji vyetu, sasa tunakwenda vitongojini”

Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa chama hicho kipo imara na kinaendelea kuwahudumia Watanzania.

Amesema kuwa kutokana na sera imara zinazotekelezaka za chama hicho, kimeendelea kufikisha huduma na mahitaji muhimu kwa Watanzania

“Chama hiki wakati wote kimesimamia utekekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kinafikisha huduma ambazo wewe mtanzania kila ukiamka ni lazima uzitumie, chama hiki pia kimeendelea kusimamia amani na utulivu nchini”