Na Hadija Bagasha Timesmajira Online,
Tanga
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha hadi ifikapo Julai 25 mwaka 2025 ziwe zimeweka miongozo mizuri ya kutoa mitaji kwa wabunifu wa bidhaa ili ziweze kuingia sokoni.
Pia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI kuhakikisha zinaweka mfumo mzuri wa kufuatiliaji na kutathimini mfumo wa sera ya elimu na mafunzo pamoja na mitaala iliyoboreshwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo Mei 31,2024 kwenye kilele cha maonesho ya wiki ya elimu, ujuzi na ubunifu yaliyofanyika Kitaifa mkoani Tanga.
“Lakini pia naomba nisistize, Wizara na Taasisi zingine za umma na binafsi ambazo zinahusika na utekelezaji wa sera hii wahakikishe kuwa na wao wanatimiza wajibu wao ipasavyo,” amesema.
Aidha ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaandaa na kukamilisha madawati ya sayansi na tekinolojia na ubunifu.
“Sambamba na hilo, suala la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanakuwa kwenye mipango yenu na yanaingizwa kwenye bajeti zenu ndani ya halmashauri zenu Kila mwaka ili yaweze kuhudumia vijana wa Kitanzania ambayo yanajishuhulisha na ubunifu,” amesema.
Sanjaru na hayo ameziagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI, kuhakikisha ifikapo Julai 2025, shule zote za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu na vyuo vya maendeleo ya jamii viwe vimeshaanzisha madawati ya sayansi na tekinolojia.
“Ili mkiamua kufanya majukwaa ya sayansi ya kiwilaya basi shule za msingi na sekondari ziweze kushiriki na kuonesha bunifu zao,”amesisitiza.
Aidha ameziagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia pamoja na TAMISEMI, kuandaa mpango madhubuti wa uandaaji na upimaji wa vituo vya umahiri vya utafiti vilivyopo nchini kwa lengo la kujihakikishia kwamba vinaendelea vizuri nà kwa tija.
“Vituo vya umahiri vya utafiti na Ubunifu vifanye kazi zao kwa viwango vya juu ili kukihitajika majibu viweze kujibu matatizo ya kijamii na kiuchumi,” amesisitiza.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema maonesho hayo yamepata mwamko mkubwa kutoka kwa wadau yakihusisha washiriki zaidi ya 140 ambao wenye bunifu na teknolojia mbalimbali zenye sifa na zinazojibu changamoto za kijamii.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi