January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini, Wang Ke, Ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 10, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Majaliwa akutana na Balozi na China, Wang Ke

Na Mwandishi Wetu,

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Wang Ke na ameishukuru Serikali ya nchi hiyo kwa misaada ambayo imetoa katika kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaotokana na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19).

“Tunaishukuru Serikali ya China kwa misaada ambayo imetupatia hadi sasa vikiwemo dawa na vifaa tiba. Na leo umesema kwamba kuna asasi za kiraia na wafanyabiashara bado wanakusanya vifaa vingine ili viletwe hapa nchini vitusadie kuzuia maambukizi, tunawashukuru sana.”

Waziri Mkuu ametoa shukrani hizo leo (Ijumaa, Aprili 10, 2020) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma alipokutana na Balozi huyo. “Mchango wenu ni muhimu sana kwetu, kwa sababu tunaanza kupata uzoefu wa namna ya kupambana na ugonjwa huu,” amesema.

Amesema Tanzania Bara na Zanzibar zinapata wagonjwa kwa sababu ni vituo vya biashara lakini wageni wote wanaoingia nchini kwa sasa wanawekwa sehemu maalumu ambako wanapatiwa huduma zote wakiwa hukohuko.

“Tunashukuru Watanzania wa pande zote mbili wanaendelea kupokea maelekezo wanayopewa, wanaendelea kujikinga na kuchukua tahadhari za kutozunguka ovyo ili wasisambaze maambukizi,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa China kwa niaba ya Serikali ya nchi hiyo kwa jinsi ambavyo waliwahudumia wanafunzi wa Kitanzania zaidi ya 500 wanaosoma China katika kipindi chote cha kupambana na ugonjwa huo.

“Balozi Mbelwa Kairuki amekuwa akitupa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na jinsi mlivyowasaidia wanafunzi wetu walioko huko na kuhakikisha wanakuwa salama tangu maambukizi yasambae nchini China.”

“Leo hii Tanzania tumeanza kupitia tatizo lile lile ambalo liliwapata ninyi. Tuna wagonjwa wachache lakini tuna kundi kubwa la wale waliokutana na wagonjwa na bado tunaendelea kuwafuatilia na kuwapima kila siku.”

“Tunaendelea na jitihada za kuzuia maambukizi mapya, tunatoa elimu kwa wananchi wetu na kuwaelimisha kuhusu kunawa mikono na kutumia vitakasa mikono. Tunaendelea kufanya tathmini kila siku ya watu wanaopimwa. Tumezuia mikutano na mikusanyiko yote, tumefunga shule na vyuo, tumezuia michezo ili tusisambaze maambukizi.”

Waziri Mkuu amemweleza Balozi huyo kwamba kwa sasa Tanzania imefunga mipaka yake kwa sababu hata nchi jirani zimefunga mipaka yao na endapo kuna wageni wanaingia nchini, ni lazima waende kwenye isolation centres ambako wanalazimika kukaa kwa siku 14.

Kwa upande wake, Balozi Wang Ke alimfikishia salamu za shukrani Mheshimiwa Waziri Mkuu kutoka kwa Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang. “Waziri Mkuu wetu anashukuru kwa barua ya pole uliyomtumia wakati nchi yetu inapitia janga kubwa la ugonjwa wa virusi vya corona,” alisema.

Alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa kwamba nchi yake sasa hivi haina maambukizi na kwamba hivi sasa wamelenga kuzuia maambukizi mapya kutoka nje ya nchi yasiingie nchini mwao.

“Kwenye baadhi ya miji tumefungua viwanda na vimeshaanza uzalishaji wa bidhaa ili kufufua uchumi wetu. Mwaka huu ni muhimu sana kwetu kwa sababu nchi yetu ilijipangia kuwa uwe ni mwaka wa kuhakikisha kuwa hakuna kabisa umaskini (zero poverty). Kwa hiyo, tunapambana kurejesha shughuli za kiuchumi zilizoathirika kutokana na ugonjwa huu,” alisema.

Balozi Wang Ke alisema nchi yake imechagua baadhi ya nchi za Afrika ambazo inazisaidia kwa kubadilishana nazo uzoefu kupitia mikutano kwa njia ya video (video conferencing) ili ziweze kukabiliana na ugonjwa huo.

“Zaidi ya hayo, kuna misaada ya vifaa tiba kwa ajili ya Serikali ya Zanzibar na Tanzania Bara ambayo inakusanywa na asasi za kiraia na wafanyabiashara. Hii iko njiani, na ile ya Tanzania Bara itawasili wiki ijayo.”