December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa aitaka Yara kuongeza uwekezaji wa mbolea, kuinua kilimo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

WAZIRI Mkuu Kassim Mjaliwa ameitaka Kampuni ya mbolea bolea ya Yara kuongeza uwekezaji wa mbolea hapa nchini sambamba na kuinua sekta ya kilimo ili kuongeza tija na manufaa zaidi kwa mkulima.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Makao Makuu ya kampuni ya Yara yaliyopo jijini Dar es Salaam juzi pamoja mambo mengine, Majaliwa amepongeza uwekezaji uliofanywa na Kampuni hiyo sambamba na kutaka uwekezaji zaidi kwenye sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

“Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli,
imeweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili kuwa na uhakika wa
malighafi viwandani na kufanikisha azma yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Tunawapongeza Yara na wadau wengine kwa namna wanavyounga
mkono juhudi hizi za Serikali,” amesema waziri mkuu.

Amefurahishwa na juhudi za Kampuni ya Yara ya kuwasaidia wakulima
wadogo nchini katika kupunguza tatizo la ajira, kuinua sekta ya kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo pamoja na kuchangia pato la Taifa.

“Tunapohimiza uwekezaji ni miongoni mwa hatua stahidi za kuondokana na changamoto za ajira, kuinua uchumi sambamba na kuongeza pato la taifa na kujiwekea usalama wa chakula.

Tunahitaji zaidi kuongeza uzalishaji wa mazao,” amesema Waziri Mkuu. Aidha, Majaliwa alichukua fursa hiyo pia kuwahakikishia wawekezaji hapa nchini kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zilizopo katika uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi katika mbalimbali za uchumi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza katika mkutano na wadau wa sekta ya kilimo ambapo ameipongeza kampuni ya Yara Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wanaofanya katika sekta ya kilimo hapa Nchini. Kulia ni Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elisabeth Jacobsen na katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo.

“Tumeona namna Yara mnavyofanya kazi zenu katika mikoa ya Dar es
Salaam, Iringa, Mbeya, Tabora, Njombe na Kilimanjaro. Serikali
itaendelea kushirikiana nanyi kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi,” amesema.

Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini, Elisabeth Jacobsen
alisema nchi yake imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono maendeleo ya sekta ya kilimo Barani Afrika ikiwemo Tanzania.

“Afrika imekuwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula, Yara imekuwa na mipango mingi katika kuhakikisha panakuwepo na usalama wa chakula ikiwepo programu ya “Action Africa’’ ambayo imelenga kugawa mbolea bure ili kuwainua wakulima wadogo hasa katika kipindi ambacho ugonjwa wa corona umeathiri nchi nyingi duniani,’’ amesema Balozi Jacobsen.

Naye Mkrugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YARA Tanzania, Winstone
Odhiambo amesema kampuni yake itaendelea kusimamia ubora wa mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao hapa nchini sambamba kutengeneza ajira kwa Watanzania.

“Yara tutaendelea kutengeneza mbolea bora ili kuzidi kumnufaisha
mkulima lakini kuzidi kutoa ajira ambapo mpaka sasa tumetengeneza
ajira rasmi zaidi ya 60 na ajira zisizo za kudumu zaidi ya 300,’’
amesema Odhiambo.

Hivi karibuni Yara walizindua programu ya “Action Africa” katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe ambao unalenga kugawa mbolea bure kwa wakulima zaidi ya 83,000 wanatarajia kunufaika na mpango huo kwa msimu wa 2020/21.