November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa agusia makubwa ya miaka mitatu ya Rais Samia

Na Mwandishi wetu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania imeshuhudia magaeuzi na maboresho makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan.

Amesema kuwa matokeo ya jitihada hizo ambayo kwa kiasi kikubwa yameimarisha ustawi wa Watanzania yanapaswa kuungwa mkono na kila mtanzania bila kujali itikadi ya vyama vyetu. “Kazi yake kubwa tumeiona, matunda ya kazi yake yamekuwa na manufaa kwetu sote”

Amesema hayo juzi wakati wa Kongamano la Kurasa 365 za Samia lililoratibiwa na Kampuni ya Clouds Media kwenye ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lililenga kuonesha mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Madarakani.

Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia katika kipindi cha miaka mitatu ameendeleza miradi yote ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo limeanza kuzalisha umeme na kuingiza katika gridi ya Taifa, uendelezaji wa mji wa Serikali.

Miradi Mingine ni Ujenzi wa Madaraja Makubwa ya Mfano ikiwemo Kigongo-Busisi ambao ujenzi wake umefikia asilimia 85 na Ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza “Hapa Kazi Tu” ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 93 na imeshaanza majaribio.

Alisema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara katika kuendeleza diplomasia ya uchumi ambayo kwa yameiwezesha Tanzania kupanua wigo wa uwekezaji .

“Kitendo hiki cha Rais Dkt. Samia kuhamasisha mataifa ya nje kujenga urafiki wa karibu na Tanzania yametuwezesha kufanikiwa kwenye maeneo ya utalii uwekezaji, mitaji, masoko ya bidhaa, ongezeko la watalii, na utatuzi wa changamoto za kibiashara na nchi jirani”

Akizungumzia Sekta ya Elimu Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa shule za msingi katika kila kijiji kwa lengo la kumuwezesha mtoto wa Kitanzania atembee umbali mfupi kufuata shule “Sekondari tulianza na mpango wa kata na tunaendelea kuongeza shule”

Aidha, amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kufungua milango kwa sekta bnafsi kushiriki katika masuala ya maendeleo nchini “Ninataka miwahakikishie watanzania, tunaendelea kufungua mipango kwa sekta binafsi na kutengeneza sera rafiki kwa ustawi wa Taifa letu.”

Amesema kuwa Serikali imeimarisha huduma za afya kuanzia vijijini kwenye zahanati mpaka hospitali za kitaifa pamoja na ujenzi wa hospitali za kanda kwa kupeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi “Tumejenga hospitali za kanda ambazo kwa sasa zinatoa huduma hata kwa wagonjwa kutoka nchi jirani.”

Amesema katika Sekta ya Maji Rais Dkt. Samia amewekeza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji akiwa na lengo la kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na uwepo wa huduma ya maji safi na salama “Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo ya kugundua maeneo yenye maji, pamoja na mitambo ya kuchimba visima, lengo lake ni kupeleka maji kwenye kila kijiji”

Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika kukuza uchumi wa nchi yetu “Moja kati ya jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais Dkt Samia amelifanya ni kuongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo ili iweze kusimamia kikamilifu sekta hii.”

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Stephen Kiruswa amesema kuwa Sekta ya Madini ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa na kuwqletea watanzania mmoja mmoja mafanikio katika kukuza uchumi wao “Kimsingi utajiri tulionao wa madini ni mkubwa sana na tutaendelea kusimamia sekta hii kikamilifu”

Naye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu Rais Dkt. Samia amewekeza katika sekta ya afya kwa ununuzi wa vifaa vya kisasa, na ujenzi wa miundombinu ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.