March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majadiliano mapendekezo ya ufundishaji kufanyika Machi 25,2025

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

MAJADILIANO yenye Mapendekezo ya Uboreshaji wa ufundishaji, Ujifunzaji na Uelewa wa Wanafunzi katika Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara yanatarajia kufanyika Machi 25, 2025 hadi Machi 27, 2025.

Huku yakitarajiwa kuja na Mapendekezo kabambe ya  kuimarisha ufanisi wa Sekta ya Elimu Jimboni humo. 

Mbunge wa Jimbo la Musoma  Vijijini Prof. Sospter Muhongo,amefadhili na kuandaa Majadiliano hayo yatakayoangazia Sekta ya Elimu Musoma Vijijini kwa upana wake ambapo yatahudhuriwa na wataalamu akiwemo Dkt.Zabron Kengera kutoka UDSM,Dkt. George Kahangwa UDSM na Japhet Makongo Ubunifu Associates.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Machi 19, 2025, imesema kuwa, Majadiliano hayo yatafanyika Ukumbi wa Kanisa Katoliki, Mugango kuanzia Machi 25, 2025, hadi Machi 27, 2025.

“Tarehe 25 March 2025,  Asubuhi Saa 3-6 Walimu Taaluma Shule za Msingi & Sekondari. Mchana Saa 8- 11 jioni  Viongozi Watendaji Kata (WEO  Afisa Elimu Kata. Na  Machi 26,  2025,
Asubuhi: Saa 3-6: Shule za Msingi Headteachers/Headmistresses. Mchana Saa 8- 11: Shule za Sekondari Headmasters/Headmistresses.”imeeleza sehemu ya Taarifa hiyo na kuongeza.

“Tarehe 27 Machi  2025 , Asubuhi Saa 3 -6  Mapendekezo kuwasilishwa
DC, DED, DEOs, Madiwani
Mbunge wa Jimbo. Mchana: Saa 8- 11 (Majumuhisho)  Mgeni Rasmi  Mkuu wa Wilaya ya Musoma  Juma Chikoka atatoa  maelekezo ya utekelezaji wa Mapendekezo.”

Aidha, Motisha zitatolewa siku ya kuhitimisha majadiliano hayo Machi 27, 2025,  kwa waliofanya vizuri mwaka 2024,  Wahusika ni Waalikwa wakiwemo Viongozi wa shule zote, Afisa Elimu Kata,Watendaji wa Vijiji (VEO),Watendaji wa Kata (WEO),Viongozi wa Halmashauri,Madiwani na  Mbunge wa Jimbo hilo.

Kwa upande wao Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wakizungumza na Majira Online wamesema katika majadiliano hayo ,  wanaamini yatakuja na mikakati mbalimbali ikiwemo  ya kuongeza ufaulu wa Wanafunzi kwa Masomo ya Sayansi na mbinu bora  za ufundishaji wa masomo hayo.

“Namshukuru Prof. Muhongo kuandaa Jambo hili bora kabisa kwa ajili ya Sekta ya Elimu Jimboni mwetu, amegusa wadau wote,  Jambo zuri Madiwani ambao ni Wawakilishi wa Wananchi watahudhuria Majadiliano hayo,  changamoto za Wananchi naomba waziweke wazi zipatiwe ufumbuzi  lipo suala la chakula shuleni baadhi ya Wazazi kuchangia ni wazito likiwekewa mikakati madhubuti  litasaidia ufaulu kwa Watoto wetu.” amesema John Masatu Mkazi wa Kijiji cha  Bukumi. 

“Mbunge wetu anafanya kazi kubwa na nzuri ya kushirikiana na Wananchi kujenga maabara, anapiga harambee kwa juhudi zote  na wakati mwingine anatumia pesa zake binafsi kulipa  Walimu wa Muda wanaofundisha Masomo ya Sayansi katika shule Mbalimbali jimboni mwetu.  Itapendeza pia kuona serikali inaleta Walimu wa Sayansi waje wasaidie kufundisha watoto wetu masomo hayo ambayo wigo wake ni mpana katika Soko la ajira na kujiajiri pia.”amesema Meshack Juma Mkazi wa Kijiji Etaro.