December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi:Upatikanaji wa maji kuongezeka kwa asilimia 87 Songwe

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Momba.

SERIKALI imeeleza kuwa upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe unatarajia kuongezeka kutoka asilimia 51 mwaka huu wa 2024 hadi kufikia asilimia 87 ifikapo Disemba 2025.

Kadhalika imesema, mpaka sasa jumla ya wakazi 133,612 katika vijiji 30 vya Wilaya ya Momba sawa na asilimia 51 wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kutumia vyanzo vya maji ya mtandao wa mabomba na visima.

Hayo yamesemwa leo Machi 20 2024, na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi katika hafla ya kukabidhi kisima kwa wananchi wa Kijiji cha Ipumpila wilayani humo, hafla iliyoenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya maji.

Mhandisi Mahundi amesema kisima hicho kimechimbwa na serikali kwa gharama ya shilingi Milioni 41, hii ni pamoja na kuweka miundombinu ya kutoa maji na kwamba katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Wilaya ya Momba imetekeleza jumla ya miradi 17 yenye thamani ya shilingi 5,113,433,491 ambayo inayohudumia vijiji 20.

“Miradi hii imeongeza hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Momba kwa asilimia 32.53 kutoka asilimia 18.47 mwaka 2020 na kufikia asilimia 51 mwaka 2024″amesema Mahundi

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Wilaya Momba, Beatus Katabazi akizungumzia mradi wa kisima katika Kijiji hicho cha Ipumpila , amesema mradi huo umetekeleza kwa gharama ya shilingi milioni 41.94 na unatarajia kuwanufaisha jumla ya wakazi 2418.

Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya ujenzi wa miundombinu midogo ya maji (Point Source 23) inayoendelea  kujengwa katika Wilaya ya momba kwa gharama ya shilingi Milioni 285 kati ya shilingi Milioni 500 zilizopelekwa na serikali wilayani humo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mateo Chikoti, amepongeza jitihada za serikali katika kushughulikia changamoto ya maji katika Wilaya ya Momba ambapo amesema mwaka 2019 kulikuwa na vijiji sita pekee vinavyopata maji, lakini hadi kufikia sasa jumla ya wakazi133,612 wanapata huduma ya maji safi na salama.

Hata hivyo Serikali katika mwaka wa fedha 2023/24 inaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya Msangano (8 vijiji), kamsamba (vijiji 2), Isanga (2) na inategemea kusaini  mikataba miradi ya  kapele (2) , Tontela (vijiji 3 ) pia inaendelea na uchimbaji wa visima virefu katika jimbo hilo pamoja na kujenga miradi ya visima ( point source 23 )  miradi hii yote itagharimu zaidi ya shilingi 13,756,289,635.