January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi: Miradi ya maji haitakuwa na maana kama vyanzo vya maji vinaharibiwa

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema fedha za miradi ya maji zinazopelekwa na serikali vijijini hazitakuwa na maana kama vyanzo vya maji vitakauka kutokana na wananchi kuharibu mazingira.

Mhandisi Mahundi ametoa kauli hiyo Januari 7,2024 baada ya kuelezwa kuwa baadhi ya wananchi wa Kata ya Kwai, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wameng’oa mabango yanayokataza watu kulima ama kufuga mifugo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vyanzo vya maji.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwemakame, Kata ya Kwai wilayani Lushoto

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kwemakame, Kata ya Kwai, ambapo amesema kuwa wananchi washirikiane kutunza vyanzo vya maji na ikibidi watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua.

“Rais Samia analeta fedha nyingi vijijini kwa ajili ya kuweka miundombinu ya maji, lakini fedha hizo hazitakuwa na maana kama wananchi wataendelea kuharibu mazingira sababu maji hayatapatikana hivyo usije ukaharibu chanzo cha maji kwa madai eneo hilo umerithi kutoka kwa mababu zako huo ni ubinafsi,”amesema .

Hivyo ameeleza kuwa mtu akiendelea kulima hapo ataumiza watu wengi ni afadhali aache kulima ili waathirike watu 10, kuliko kulima na kuathiri watu 500.

Akiwa Kata ya Kwekanga amewaeleza wananchi kuwa tambiko kubwa ni kulinda mazingira na sio kuchinja kondoo na njiwa ili kuvifanya vyanzo vya maji visikauke.

Wananchi wa Kijiji cha Kwemakame, Kata ya Kwai wilayani Lushoto wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (hayupo pichani)

Ambapo kauli hiyo ameitoa baada ya kuelezwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kuwa wazee wa kata hiyo waliomba RUWASA na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi kuwapelekea kondoo na njiwa ili wakatambikie eneo ambalo maji yalikauka kimiujiza.

“Rais hataki wanawake wateseke kwa kubeba ndoo kichwani amenunua magari 25 nchi nzima yenye mitambo ya kuchimba maji,Mkoa wa Tanga pia umepata gari hilo, linakuja Lushoto wiki ijayo baada ya kuwa Msomela, Handeni kwa kazi maalumu lakini maji ya kuchimba kwa visima yana gharama kubwa, tofauti na yale ya mtiririko kutoka milimani,”amesema Mahundi.

Akiwa Kata ya Makanya, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itachimba visima viwili ambavyo vitatosha kuhudumia wananchi wa vijiji vitano vya kata hiyo sababu watajenga matenki na miundombinu ya mabomba ili kusambaza maji hayo, huku akionya kama wananchi wataendelea kuharibu mazingira, hata maji yaliopo ardhini yatakauka.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Kata ya Kwekanga, Shekilindi alikiri kutoa sh. 150,000 kwa wazee hao wa kata hiyo ili wakafanye tambiko ikiwa ni pamoja na kuwaongezea kondoo mmoja kati ya wawili waliohitajika kwa kazi hiyo ili kurudisha vyanzo vya maji vilivyokauka kimiujiza, lakini hakukuwa na mafanikio yeyote.

Mabomba yakiwa Kijiji cha Kwekanga, Kata ya Kwekanga, wilayani Lushoto. Mabomba hayo yalipelekwa kwa ajili ya Mradi wa Maji Kwekanga, lakini baada ya chanzo walichokuwa wanakitegemea kukauka, mabomba hayo yatatumika kwenye Mradi wa Visima Kijiji cha Kwekanga.

Awali, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Sizinga amesema Kata ya Kwai wananchi wanang’oa mabango yanayoonesha eneo husika ni chanzo cha maji, huku kata za Kwekanga na Makanya hazina miradi ya maji kutokana na kukosa vyanzo vya maji.

Lakini wana mpango wa kukarabati mradi wa maji Kwemakame uliojengwa zaidi ya miaka 40 iliyopita, huku Kata ya Kwekanga wakiwa wameshapeleka mabomba kwa ajili ya maji ya visima.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (kulia) akimkabidhi sh. 850,000 Diwani wa Kata ya Makanya Zaniali Salehe (kushoto). Mahundi alianzisha harambee na yeye kutoa sh. 300,000 baada ya kuombwa na diwani huyo kuchangia ujenzi wa Shule Shikizi ya Shule ya Msingi Makanya