Ataka wakandarasi nchini kumaliza miradi kwa wakati
Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Lushoto
NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi alifanya ziara ya siku nne (4) kwenye Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga. Na aliweza kutembelea majimbo yote matatu ya wilaya hiyo ikiwemo Jimbo la Lushoto, Bumbuli na Mlalo.
Ziara hiyo ilibeba mambo mengi ikiwemo kukagua miradi ya maji ambayo utekelezaji wake unaendelea. Kupata taarifa ya miradi inayofanyiwa usanifu, kufika maeneo ambayo kuna miradi ya zamani, na imekuwa chakavu, ili kuona inafanyiwa ukarabati mkubwa, kufika maeneo ambayo hakuna kabisa miradi ya maji ili kuona namna ya kuwapatia wananchi miradi ya maji.
Lakini pia, kufanya mikutano ya hadhara ili kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za maji, na kuwaeleza wananchi jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, namna ya kumtua ndoo kichwani mwanamke wa Kitanzania.
Mwandishi wa makala haya alikuwepo kwenye ziara hiyo iliyoanza Januari 6 hadi 9, 2024, na alifuatilia maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri, na mipango inayofanywa na Serikali kwa kuweza kufikisha maji kwa asilimia 85 vijijini, huku mijini ikiwa ni asilimia 95 ifikapo mwaka 2025
Akiwa kwenye Mradi wa Maji Magamba Lushoto eneo la chanzo cha maji (Intake) Kibohelo, Mahundi alimtaka Mkandarasi anaejenga Mradi wa Maji Magamba Lushoto Mjini, M/S PNR Services Ltd wa mkoani Dar es Salaam, kukamilisha mradi huo Aprili, mwaka huu, kwani hawataweza kumuongezea muda mwingine.
Kipande anachotakiwa kukamilisha ni cha bomba kubwa lenye kipenyo cha inchi 12 la kutoa maji kutoka chanzo cha maji kilichopo Kibohelo hadi lilipo tenki la maji, Magamba Cost lenye urefu wa kilomita 5.4
“Natoa agizo, na hili ni kwa wakandarasi wote nchini. Hatutaongeza muda wa kukamilisha miradi ya maji. Tunataka miradi ya maji ikamilishwe kwa wakati ili wananchi wapate maji. Na tunataka viongozi wanapokwenda kukagua miradi wapate majibu ya kutosheleza kuhusu utekelezaji wa mradi.
“Hivyo, hatutaweza kumuongezea muda tena Mkandarasi anaejenga Mradi wa Maji wa Magamba Lushoto Mjini. Tunataka akamilishe mradi Aprili, mwaka huu kwa kukamilisha kazi zilizobaki ikiwemo ujenzi wa bomba kubwa la kutoa maji kwenye chanzo hadi kwenye tenki. Nia yetu ni kuona kuanzia Aprili, mwaka huu wananchi wa Mji wa Lushoto wanapata maji ya uhakika” anasema Mhandisi Mahundi.
Naibu Waziri, pia alitembelea Mradi wa Maji Irente- Yoghoi- Ngulwi- Bombo uliopo Kata ya Ngulwi, ambapo baada ya kupokea malalamiko ya upendeleo wa mgao wa maji, aliagiza RUWASA kuendelea kusimamia Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s), na kuagiza kubadilisha wafanyakazi wanaogawa maji kwenye eneo hilo ili kuweka wengine watakaogawa maji kwa usawa.
Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Ubiri na Gare, Mhandisi Mahundi aliahidi kuzitafutia maji ya uhakika kata hizo, huku akiahidi wananchi wa vijiji vya Miegeo na Handei kwenye Kata ya Ubiri kupata maji ndani ya wiki moja kutoka kwenye Mradi wa Maji Ngulwi, huku Kata ya Gare ikichimbiwa visima kabla ya kusubiri mradi mkubwa wa maji ya bomba ya kata 13.
Akiwa Kijiji cha Kwemakame, Kata ya Kwai, Mahundi anasema fedha za miradi ya maji anazopeleka vijijini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hazitakuwa na maana kama vyanzo vya maji vitakauka kwa wananchi kuharibu mazingira.
Ni baada ya kuelezwa kuwa baadhi ya wananchi wa Kata ya Kwai, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wameng’oa mabango yanayokataza watu kulima ama kufuga mifugo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vyanzo vya maji, na kuwataka wananchi washirikiane kutunza vyanzo vya maji, na ikibidi watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analeta fedha nyingi vijijini kwa ajili ya kuweka miundombinu ya maji, lakini fedha hizo hazitakuwa na maana kama wananchi wataendelea kuharibu mazingira sababu maji hayatapatikana.
“Usije ukaharibu chanzo cha maji kwa madai eneo hilo umerithi kutoka kwa mababu zako, sababu huo ni ubinafsi. Ni kweli umerithi, lakini ukiendelea kulima hapo utaumiza watu wengi. Ni afadhali uache kulima ili waathirike watu 10, kuliko kulima na kuathiri watu 500” anasema Mahundi.
Akiwa Kata ya Kwekanga aliwaeleza wananchi kuwa tambiko kubwa ni kulinda mazingira, na wala sio kuchinja kondoo na njiwa ili kuvifanya vyanzo vya maji visikauke.
Ni baada ya kuelezwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kuwa wazee wa kata hiyo waliomba RUWASA na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi kuwapelekea kondoo na njiwa ili wakatambikie eneo ambalo maji yalikauka kimiujiza.
“Tambiko kubwa ni kutunza mazingira, na wala sio kuchinja kondoo. Acheni kulima kando ya mito na vyanzo vya maji. Acheni tambiko la Mungu lifanye kazi yake kwa ninyi kuacha kulima kwenye vyanzo ili uoto wa asili uweze kurudi, halafu hilo tambiko la kondoo mtaendelea nalo.
“Nataka kuwaeleza, Rais Dkt. Samia anawapenda wananchi wake, na hataki wanawake wateseke kwa kubeba ndoo kichwani, hivyo amenunua magari 25 nchi nzima yenye mitambo ya kuchimba maji, na hata Mkoa wa Tanga umepata gari hilo, na linakuja Lushoto wiki ijayo baada ya kuwa kule Msomela, Handeni kwa kazi maalumu. Lakini maji ya kuchimba kwa visima yana gharama kubwa, tofauti na yale ya mtiririko kutoka milimani” anasema Mahundi.
Akiwa Kata ya Makanya, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itachimba visima viwili ambavyo vitatosha kuhudumia wananchi wa vijiji vitano vya kata hiyo sababu watajenga matenki na miundombinu ya mabomba ili kusambaza maji hayo, huku akionya kama wananchi wataendelea kuharibu mazingira, hata hayo maji yaliyopo ardhini yatakauka.
Akiwa kwenye kukagua miradi ya maji Funta na Wanga, Mahundi amewataka wanasiasa wasije wakaposha juu ya huduma ya maji, na badala yake waseme ukweli kwa wananchi kuwa huduma ya maji inalipiwa ili miundombinu ya maji iweze kuwa endelevu.
Anasema ni kweli maji ni ya Mungu, lakini yakichakatwa ili kuwafikia wananchi, kuna gharama, lakini gharama hizo, tayari zimebebwa na Serikali kwa kupeleka miradi hiyo kwa wananchi, lakini ili miradi hiyo iwe endelevu, wananchi lazima walipie huduma ya maji.
“Serikali imedhamiria kupeleka maji kwenye kila kijiji, na kwenye kila kitongoji, na ifikapo mwaka 2025, maji hayo yapatikane kwa asilimia zaidi ya 85. Lakini tukiweka maji hayo John atafungua koki hiyo, Hassan atafungua koki hiyo, Halima atafungua koki hiyo, mara ng’ombe amepita, amepiga pembe koki hiyo, hivyo itavunjika.
“Sasa ili kuweza kununua koki nyingine na mabomba yaliyoharibika au kuwa chakavu, itabidi tuchangie. Kila familia ikichangia sh. 5,000 (Mwangozo wa Wizara maji ya mserereko), mradi utakaa hadi miaka 50 au 100. Hivyo, viongozi wa kisiasa waseme ukweli kwa wananchi kuwa maji yanalipiwa, wasitake kujitengenezea mazingira ya kuchaguliwa kwa kupotosha wananchi kuwa wasilipe… usiseme sh. 1,000 sitoi, mradi utakufa” anasema Mahundi.
Mahundi anasema wanataka wananchi wachangie huduma ya maji kutokana na makubaliano kwenye vikao vyao vya vijiji vilivyoamua ama kupanga vikishirikiana na Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s).
Alipokuwa Kata ya Rangwi, Mahundi amewataka wananchi wa Kijiji cha Goka kuacha kujiunganishia maji kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki, kwani kufanya hivyo, kunawanyima fursa ya kupata maji wananchi wa vijiji vingine vitano vya kata hiyo.
Alielezwa kuwa wananchi hao wametoboa bomba kuu na kuchukua maji kwa nguvu kwa ajili ya matumizi ya kunywa na kunyweshea mashamba yao kwa madai maji hayo chanzo kipo kwao, lakini mtandao wa mabomba unakwenda kwa vijiji vingine.
Mahundi anasema hakukuwa na sababu wananchi hao kujiunganishia maji kwenye bomba kuu linalopeleka maji kwenye tenki, na badala yake wangeomba na wao wawekewe miundombinu ya maji ikiwemo mabomba na vituo vya kuchotea maji (vilula), lakini baada ya maji yote kuingia kwanza kwenye tenki.
“Wananchi wa Goka msiwe wabinafsi kwa kujiunganishia maji kutoka kwenye bomba kuu kabla ya kuingiza maji kwenye tenki. Mnatakiwa mruhusu maji yafike kwanza kwenye tenki kuanzia lile bomba kuu, pamoja na bomba la nchi tatu lililowekwa na CHAMAVITA. Baadae wataalamu watakuja kupima na kuangalia umbali wa kuyatoa maji kutoka kwenye tenki hadi Kijiji cha Goka.
“Na tukiruhusu maji yote yakaweza kuingia kwenye tenki vijiji vyote sita vya Kata ya Rangwi ikiwemo Emau, Rangwi, Nkelei, Karumele, Goka na Mambo vitapata maji” anasema Mahundi.
Mahundi, pia aliwasifu wananchi wa Kijiji cha Goka kwa kuweza kukilinda chanzo hicho cha maji tangu kujengwa kwa mradi huo miaka 46 iliyopita, lakini akataka waongeze jitihada za kukitunza sababu pale kwenye bomba lililowekwa na CHAMAVITA, chanzo kina maji mengi, lakini pale lilipo bomba kuu, chanzo kimepungua.
“Tunaomba muendelee kuiamini Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani, na watahakikisha ifikapo mwaka 2025, wananchi watapata maji kwa asilimia 85, huku mijini wakipata kwa asilimia 95” anasema Mahundi.
Akiwa Kijiji cha Masereka, Kata ya Mbaru, Mahundi aliwaeleza wananchi wa kata hiyo kuwa anafahamu shida ya maji waliyonayo, na hiyo inatokana na yeye kuulizwa maswali bungeni na Mbunge wa Jimbo la Mlalo Rashid Shangazi.
Mahundi anasema wataweza kupeleka maji hapo kwa njia mbili, aidha kwa kutumia chanzo cha maji Goka, ama kuchimba visima, kuweka kwenye matenki, na kusambaza maji hayo kwa mtandao wa mabomba.
Kwenye kikao cha majumuisho kilichofanyika Ofisi ya RUWASA Wilaya ya Lushoto, Mahundi aliwapa moyo wafanyakazi wa RUWASA na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Lushoto (LUWASA), kuwa wanafahamu kazi na mazingira wanayofanyia kazi.
Na hata wanapowahimiza kufanya kazi kwa bidii, ni kuwataka waongeze uwajibikaji ili kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati, na wananchi wanapata maji kwa wakati, kwani wao kuanzia Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ndiyo wamepewa dhamana ya kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani.
FEDHA NA MIPANGO
Kwenye taarifa ya hali ya huduma ya maji, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga anasema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Wilaya ya Lushoto imetengewa sh. 3,654,137,228 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mipya, upanuzi wa miradi, ukarabati pamoja na uandaaji wa miradi na usimamizi wa miradi, ambapo mpaka kufika Desemba, 2023, Wilaya ya Lushoto imepokea jumla ya fedha sh. 2,443,502,496 kati ya sh. 3,654,137,228, hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 66.9 ya fedha zote za bajeti kwa mwaka huo wa fedha.
UWEKEZAJI WA MIRADI
Mhandisi Sizinga anasema kwa sasa Wilaya ya Lushoto ipo katika ujenzi wa miradi ya maji kama ifuatavyo. Ujenzi wa Mradi wa Maji Lushoto Mjini [Magamba] sh. 1,800,919,263, ujenzi wa Mradi wa Maji Ngulwi sh. 578,175,639, ujenzi wa Mradi Maji wa Tewe sh. 454,893,687, ujenzi wa Mradi wa Maji Mkundi Mbaru/Mtae sh. 787,204,963, ujenzi wa Mradi wa Maji Gologolo/Hemtoye sh. 1,353,414,436.
“Ujenzi wa Mradi wa Maji Msamaka sh. 1,294,128,433, ujenzi wa Mradi wa Maji Kisiwani sh. 437,719,428, ujenzi wa Mradi wa Maji Makole/Kilole/Kwekanga sh. 337,874,430, ujenzi wa Mradi wa Maji Milingano sh. 339,106,904, ujenzi wa Mradi wa Maji Kwediwa sh. 285,356,892, ujenzi wa Miradi ya Maji Kiluwai/Kidunda, Funta na Wanga sh. 2,702,000,937” anasema Mhandisi Sizinga.
Ameongeza kuwa kuna Usanifu wa Miradi mbalimbali unaofanywa na Kampuni ya Mtaalam Mshauri Envy Consult kwa miradi ya Mnazi, Mng’aro, Lunguza, Soni, Gare, Magamba kwenda kata za Migambo, Kwai (Kwemakame), Kwekanga na Makanya sh. 201,498,129,
Kufanya survey na uchimbaji wa visima virefu kwa maeneo ya Makole, Kwekanga, Mlola, Makanya sh. milioni 300.
Anasema miradi yote ina vyanzo vya maji vya mserereko vyenye maji mengi na ya kutosha hivyo mategemeo ni kuwa miradi yote itakamilika na kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wilaya ya Lushoto.
“Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, na ina gharama ya sh. 10,872,293,144, na ikikamilika itanufaisha wakazi 85,655 wanaoishi maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Lushoto, sawa na asilimia 16.7 ya wakazi wote wanaoishi wilaya hii. Miradi hii ikikamilika itaongeza kiasi cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 72.1 ya sasa mpaka kufikia asilimia 88.8” anasema Mhandisi Sizinga.
UTOAJI WA HUDUMA YA MAJISAFI
Mhandisi Sizinga anasema kwa sasa huduma ya maji kwa maeneo ya Mji wa Lushoto inatolewa na Mamlaka ya Maji ya Lushoto kwa kushirikiana kwa karibu na RUWASA. Mamlaka hii inasimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Kwa maeneo ya vijijini huduma ya maji inatolewa na Bodi za Maji kwa ngazi ya Jamii (CBWSO’s). Mpaka sasa Wilaya ya Lushoto ina jumla ya Bodi za Maji saba tu ambazo zimeunganishwa kwa mujibu wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019.
“Aidha, Ofisi ya RUWASA inaendelea kutoa elimu kwa jumuiya zote ili zione umuhimu wa uendelezaji wa miradi ya maji na kuacha mazoea na zana potofu ya kuwa maji ni mali ya Mungu, hivyo hayapaswi kulipiwa. Kwa sasa maeneo mengi ya Wilaya ya Lushoto bei za maji ni kwa makadirio (flat rate), ambapo kwa wastani bei ya maji kwa mwezi ni sh. 1,000 hadi 5000” anasema Sizinga.
UTHIBITI UBORA
Katika utekelezaji wa miradi ya maji, vifaa vyote vinavyotumika kwenye ujenzi vilichukuliwa vipimo na maabara ili kutambua ubora wake, kwa sasa sample za maji zimekusanywa ili kujua ubora wake kwa kipindi hiki cha robo ya kwanza na ya pili kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
MAZINGIRA
Miradi ya Maji iliyopo katika Wilaya ya Lushoto inatoa maji yake kwenye vyanzo ambavyo vinatunzwa vizuri na Sekta ya Misitu na Maliasili. Hali hii imeifanya miradi mingi kutokuwa na athari za kimazingira, kwani bomba za maji zinapita msituni, ambapo hakuna athari za kimazingira. Bado maeneo machache wananchi wamekuwa na changamoto ya kufanya sughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ikiwemo kilimo, ufugaji na uchimbaji wa madini.
CHANGAMOTO
Kumekuwa na changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zinazosababisha kazi kufanyika kwa kasi isiyoridhisha. Miundombinu chakavu kwa maeneo mengi ya vijijini, miradi ya muda mrefu, mwamko mdogo wa wananchi kulipia huduma ya maji, na shughuli za kibinadamu maeneo yenye vyanzo vya maji.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele miradi ya maji kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji kwa Wilaya ya Lushoto. Hali hii imefanya hali ya huduma katika maeneo mengi kuimarika zaidi” anasema Mhandisi Sizinga.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika