Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MGANGA Mkuu wa Jiji la Dodoma Andrew Method amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kliniki hadi wanapofikisha umri wa miaka mitano kwani ni kipindi ambacho wataalam wanaendelea kufuatilia afya ya mtoto ili kumwezesha kufikia ukuaji timilifu.
Dkt.Method ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu huduma za kliniki zinavyoweza kuchangia kuboresha afya ya mtoto na kumwezesha kukua vyema na kufikia utimilifu wake.
Amesema,ni muhimu mtoto kuhudhuria kliniki ili kujua maendeleo ya afya yake ambapo atakushauriwa nini cha kufanya kama afya ya mtoto inasuasua ambapo huweza kusababisha afya ya mtoto kuyumba na kuwa katika hatari ya kupata ukondefu au udumavu hali inayoathiri ukuaji wa mtoto.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Mkoa wa Dodoma Ally Mvungi amesema,hivi sasa huduma za kliniki (kadi) zimeboreshwa ambapo kwa sasa kuna kipimo cha kuangalia ukondefu tofauti na kadi za zamani ambazo zilikuwa zinaangalia uwiano wa uzito na umri wa mtoto ambapo kwa kiashiria hicho kimeonekana kufanya vizuri wakati kipimo cha ukondefu na udumavu hakikupatikana.
Kwa upande wake Amina Abubakar (mzazi) amesema,suala la wazazi au walezi kuwapeleka watoto kliniki hasa anapokuwa amemaliza chanjo ni changamoto kutokana na ubize wa wazazi au kuona kama haina maana tena.
“Mimi ni mmoja wa wazazi ambaye niliacha kumpeleka mwanagu kliniki alipofika miaka minne,na hii nilifanya hivyo baada ya kuona hakuna umuhimu sana kuendelea kumpeleka kliniki kwani alikuwa ni mkubwa na chanjo alishamaliza.”amesema Amina
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba watoa huduma za afya waendelea kutoa elimu ya mara wa mara kuhusu umuhimu wa watoto kupelekwa kliniki na kwamba ni moja ya eneo linalochangia kuboresha afya ya mtoto.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Halima Kassim amesema zipo athari nyingi zinazoweza kumpata mtoto endapo hatahudhuria kliniki kwa sababu hilo ni eneo ambalo watalaam wanapima maendeleo ya afya yake na makuzi ya mtoto.
“Lakini pia mtoto anapoenda kliniki anapata chanjo kwa ajili ya kumpa kinga za mwili wake kumkinga na maradhi mbalimbali na pia kingine kujua maendeleo ya makuzi yake.” Amesema na kuongeza kuwa
“Tusipompeleka mtoto kliniki hatopata chanjo kwa ajili ya kinga yake lakini hatutaweza kujua maendeleo yake na kujua maendeleo ya makuzi yake kwa ujumla,pia hatoweza kugunduliwa kama kuna maradhi yanayomnyemelea mtoto ambapo yangegundulika mapema angeweza kutibiwa na kuepusha madhara yatokanayo na kugundua changamoto ya kiafya na kuitatua kwa haraka.”
Kwa upande wake Muuguzi Msaidizi hospitali ya Makole jijini Dodoma Josephine Dikoko amesema Mtoto chini ya miaka mitano asipohudhuria kliniki athari zake ni kutokuwa na ukuaji mzuri ,mtoto kuwa hatarini kupata magonjwa yanayozuilika kwa chanjo .
Dikoko ameyataja magonjwa yanayoweza kumpata mtoto asiyepata chanjo kuwa ni pamoja na kifua Kikuu,ugonjwa wa kupooza(polio), ugonjwa wa kuharisha,homa ya uti wa mgongo,Pepo punda,kifaduro,Dondakoo,surua,Homa ya ini,Homa ya kichomi,magonjwa ya kuhara lakini pia mtoto anaweza kupoteza maisha.
“Magonjwa haya yanaathiri ukuaji wa mtoto kwa sababu ili mtoto akue vizuri ni lazima awe na afya njema ,lakini mtoto anayeandamwa na maradhi mara kwa mara hawezi kukua vizuri,maana hata lishe yake pia itakuwa duni,pia mwili wake utakuwa dhaifu ,kwa mantiki hiyo hawezi kukua vizuri.”amesema Dikoko na kuongeza kuwa
“Pia anakuwa hana kinga ya kutosha mwilini hivyo basi atakuwa anaandamwa na maradhi mara kwa mara na hivyo kuathiri ukuaji wa ubongo wake.”
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi