December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maharage :Mradi Bwawa la Nyerere utafikia asilimia 91 Septemba

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline, Rufiji.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa tathmini ya ukamilikaji wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), uliopo Mkoani Rufiji, kuwa mradi huo unaendelea vizuri na hadi kufikia Mwezi Septemba unatarajia kufikia asilimia 91.

Akizungumza na Waandishi wa habari, alipotembelea mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande, amesema, hadi sasa mradi huo unaendelea vizuri, ambapo kwa sasa umefikia asilimia 90.19 na wakati wowote baada ya kukamilika kwa miundombinu ya ujenzi umeme utaanza kuzalishwa.

Chande amesema, kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa mradi huo na kuwa na maendeleo mazuri, hadi kufikia Mwezi Juni, 2024, mradi huo unatarajiwa kuanza kuzalisha umeme nchini.

“Tumeamua kutembelea mradi huu kwa ajili ya kuangalia tathmini ya mradi na kama mnavyoona mradi unaendelea vizuri kwani hadi Mwezi Julai mradi ulifikia asilkmia 90.19 na tunatarajia hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu Agosti kwa maana ya mwanzoni mwa mwezi Septemba tutakuwa tumeifikia 91% kwa mantiki hiyo hadi kufikia Mwezi Juni 2024 tayari umeme utakuwa unazalishwa hapa”,amesema Chande.

Pia amesema kuwa, hadi sasa idadi ya wafanyakazi imeongezea nakufikia 20, lengo likiwa ni kuongeza nguvu kazi katika mradi huo na kuongeza kuwa hivi sasa mradi huo upo katika hatua za ukamilishwaji wa ujenzi wa kimiundombinu na ufungaji wa mitambo.

Vilevile ametolea ufafanuzi wa mahitaji ya umeme kwa wananchi, amesema ndani ya miaka miwili 2022/2023 mahitaji ya umeme ya juu yameongezeka hadi kufikia zaidi ya Megawat 100 tofauti na vipindi vingine.

“Kama mnavyofahamu, kwa mwaka jana mahitaji ya umeme ya juu yalikuwa Megawat 1354 na kufikia mwezi huu Agosti tumevunja rekodi na kufikia mahitaji ya umeme ya juu 1482 hivyo kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya umeme ya juu zaidi ya Megawat 100 hivyo mtaona mashindano ya mahitaji ya umeme yanavyoongezeka na sisi tutashinda mashindano hayo kwa kuhakikisha tunaleta umeme unaokidhi hali yetu ya uchumi,”amesema Chande.

Katika hatua nyingine, amewatoa hofu wananchi na kuwataka kuwa wavumilivu na kudai kuwa, ukamilikaji wa mradi huo utasaidia kuondoka changamoto ya ukosefu wa umeme wa mara kwa mara.