January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maharage aina ya Jesca yawa kivutio kwa wanaume kuyatumia

Na Esther Macha, Timesmajira,Majira,Online,Mbeya

ZAO jipya aina ya maharage ya Jeska limeonekana kuwa na soko kubwa kwa wakulima kutokana na wateja wake wakubwa kudaiwa ni wanaume kutokana na kuongeza nguvu za kiume na kuzibua mishipa mwilini.

Imeleezwa kuwa maharage hayo aina ya Jeska yamekuwa na madini ya zinki na chuma ambayo yamekuwa yakipendwa zaidi na jinsia ya kiume ikiaminishwa kuwa ni bora ambayo yanazibua mishipa mwilini.

Ezekia Wilson ni Ofisa Masoko na Kilimo wa Kampuni ya Rapha Group Ltd amesema hayo wakati walipotembelewa na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Akson katika banda hilo kuona shughuli zinazofanywa na kampuni hiyo.

Wilson amesema kuwa wanaamini kuwa maharage hayo yana soko kubwa kwani yanafanya kazi kubwa mwilini hasa kwa jinsia ya kiume,ni zao ambalo lina soko kubwa lakini hayalimwi kwa wingi kutokana na wakulima kutokuwa na elimu ya namna ya kuyalima maharage hayo hivyo yanaingia sokoni kwa uchache na kuwahi kuisha na hupandwa kwa awamu mbili inapofika Septemba huwezi kuyapata tena sokoni kwasababu yanakuwa yameshanunuliwa na watu.

“Hivyo tunapenda kuwashauri wakulima kuendelea kuongeza nguvu zaidi za kulima zao hilo kwa wingi aina ya maharage ya Jesca ,sisi kama kampuni ya Rapha group tunaahidi kununua maharage hayo kwa kiwango chochote ambacho mkulima atazalisha,”amesema.

Akifafanua zaidi Wilson amesema kuwa kwa mwaka 2022 walinunua tani 10 za maharage Jeska lakini mahitaji ni makubwa na kwamba mwaka huu wameweza kukusanya tani 25 za maharage ya Jesca.

Amesema kuwa zao ambalo wanazalisha kimkakati ni mpunga kwasababu kampuni hiyo inafanya asilimia 50 kwenye mpunga na mazao mengine asilimia 50 hivyo tunahamasisha wakulima zao lingine ambalo linahitajika ni maharage ya njano na kipapi na mwasipenjele.

Hata hivyo amesema maharage hayo yanauzwa nchini Malawi,Zambia,Nigeria hivyo wakulima waongeze nguvu katika kilimo hicho cha zao hilo.

Akizungumzia mkakati wa kampuni kuhusu maharage aina ya Jesca amesema kuwa imejipanga sababu soko lipo maana wanauza kwa bei wanayotaka na pia wanatarajia kusambaza mabwana shamba kwa wingi ili waweze kupata elimu.

Tusajigwe Mbula ni mkulima kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya amesema kuwa amekuwa akisikia sifa ya zao hilo jipya la maharage ya Jesca lakini bado anatamani apate elimu zaidi kutoka kwa Maofisa Ugani ili aweze kulima na kukuza uchumi.