March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakimu Majaji waaswa kufanya kazi kwa weledi

Na Joyce Kasiki, Dodoma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewataka Majaji na Mahakimu nchini kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba pamoja na sheria za nchi.

Dkt. Nchimbi amesema kuwa licha ya Mahakama kuwa na uhuru wa kikatiba katika utekelezaji wa majukumu yake, uhuru huo haupaswi kutumiwa kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo vinavyokiuka misingi ya haki.

Ameyasema hayo jijini Dodoma alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Sheria nchini.

Alisisitiza kuwa uhuru wa Mahakama ya Tanzania ni dhamana muhimu ya kulinda haki za wananchi, na kwamba unapaswa kutekelezwa kwa uwazi, uadilifu na kwa kuzingatia kikamilifu Katiba na sheria za nchi, ili kuendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa mhimili huo muhimu wa dola.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi amemshukuru Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, kwa kutoa wito kwa viongozi wa serikali kutoendelea kuikumbusha jamii kuhusu matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa kufanya hivyo ni kutonesha vidonda na kunaweza kuathiri mchakato wa upatikanaji wa haki.

Makamu wa Rais alisema anakubaliana na wito huo, lakini amekumbusha kuwa haupaswi kuwalenga viongozi wa serikali pekee, bali pia viongozi wa kisiasa, taasisi za kijamii na wanaharakati wote waliokuwa wakikumbusha matukio hayo.

Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameunda Tume ya kuchunguza kiini cha matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo imeanza kazi, hivyo kuendelea kuzungumzia matukio hayo ni kwenda kinyume na mfumo wa kisheria uliowekwa na kutolitendea haki Taifa.

“Wote wanaoipenda Tanzania wanapaswa kuukubali wito wa Wakili Mwabukusi na kuiruhusu serikali kutimiza jukumu lake kupitia Tume hiyo ya Rais,” amliema Dkt. Nchimbi.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, alisema Mahakama itachukua hatua stahiki kuhakikisha inakuwa mahali pa kupata haki kwa wakati bila ucheleweshwaji, badala ya kuwa mahali pa kuegesha mashauri ya migogoro.

Alusema baadhi ya wadau si waaminifu, kwani wanashindwa kuwajibika kimikataba na kisheria katika mashauri ya madai, hali inayosababisha ucheleweshaji wa haki.

 Amesisitiza kuwa Mahakama itachukua hatua dhidi ya wahusika ili kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa mawakili pamoja na watendaji wa mahakama.

Aidha, Jaji Mkuu ameeleza kuwa Mahakama inaendelea kuchukua hatua za kuiboresha Sheria ya Mawakili ili kulinda mamlaka na uhuru wake. Miongoni mwa hatua hizo ni kuhakikisha madalali wa mahakama (court officers) wanazingatia Katiba, sheria, maadili ya kazi pamoja na hukumu na amri za mahakama, huku wale watakaokiuka wakichukuliwa hatua za kisheria.

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, alisema ni dhana potofu kudhani kuwa ustawi na maendeleo ya taifa hufanikishwa na Serikali pekee. Amesema maendeleo ya taifa lolote hutokana na ushirikiano wa mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Amefafanua kuwa Serikali huchangia maendeleo kupitia majukumu yake ya kiutendaji, Bunge kupitia kutunga sheria na kuwakilisha wananchi, huku Mahakama ikichangia kwa kutafsiri sheria, kutunga baadhi ya kanuni na kuhakikisha mazingira wezeshi ya utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.

Kwa upande wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimesema hakiridhishwi na tabia ya baadhi ya mawakili kupokea malipo kutoka kwa wateja bila uwajibikaji unaostahili, na kusisitiza kuwa taaluma ya uwakili ni ibada yenye dhamana kubwa kwa jamii.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, amesema Shule ya Sheria (Law School) inapaswa kuchunguzwa kwa kina ili kuhakikisha michakato yake ya kuandaa mawakili inalenga kuzalisha mawakili waadilifu na wenye sifa stahiki.

Ameiomba Serikali kuimarisha shule hiyo kwa kuweka vigezo na vikwazo madhubuti vitakavyodhibiti uingizwaji wa watu wasiofaa katika taaluma ya uwakili.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Sheria mwaka huu yamefanyika katika makao makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, yakibeba kauli mbiu isemayo

 “Mchango wa Mahakama kwenye maendeleo na ustawi wa Taifa.