December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama ziongeze kasi kutekeleza maelekezo ya Samia utendaji haki

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

WIKI iliyopita nimebatika kufuatilia kinachofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kupitia utaratibu aliouanzisha kutatua kero za wananchi.

Kwa waliofuatilia kile kilichojiri kwa Makonda na yale ambayo alikumbana nayo wakati akiwa kwenye nafasi ya Uenezi ndani ya CCM, atakubaliana na mimi, kwamba nchi yetu imekubikwa na kilio cha wananchi kukosa haki.

Mwanzo nilipokuwa namsikia Rais Samia Suluhu Hassan, akiwaagiza wasaidizi wake kutatua kero za wananchi, haikuwa rahisi kuelewa ukubwa wa tatizo.

Kimsingi hali ni mbaya, wananchi wana malalamiko mengi, wengine wanatembea na hakumu zilizowapa ushindi kutoka kwenye mahakama za rufaa, lakini haki zao hawazipati. Kibaya zaidi wanaokwamisha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama ni watumishi wa Serikali.

Kimsingi, ni wazi kwamba kinachofanywa na watendaji wa Serikali na wengine kutotekeleza maamuzi ya mahakama ni dharau kubwa, pengine ndiyo maana watu wengine wanakosa imani na chombo hicho.

Kiuhalisia haina maana mtu kuwa na hukumu iliyompa ushindi kwenye makaratasi, wakati hapati haki yake na wanaokwamisha ni wasomi waliopewa dhamana kubwa Serikalini.

Pamoja na mahakama zetu kutoa uamuzi na wakati kutotekelezwa na wahusika, lakini kumekuwa na kilio kingine cha kesi kuchukua muda mrefu kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Na hili Rais Samia Suluhu Hassan, ameliona na kulitolea maelekezo, ambapo anataka Mahakama kupunguza mlolongo wa muda wa kesi za madai ili wananchi wapate haki kwa wakati.

Anasema kuchelewa kutoa haki kunapelekea watu wengi kupoteza haki zao au kuchelewa kuzipata jambo ambalo linaweza kumalizwa kwa wakati.

“Kwenye mahakama za chini kesi za madai zinakwenda hadi miezi 12 na Mahakama za Rufani hadi miezi 24, hii siyo sawa kabisa ni lazima tubadilike sasa ili watu wetu wapate haki stahiki na kwa wakati,” anasema.

Hata hivyo amesema kazi ya kutoa haki ni ya Mungu mwenyewe kwa hiyo waliopewa dhamana watende kwa haki waepuka kuwaumiza wanyonge.

Rais Samia anasema iliwalazimu kuanzisha huduma za kisheria kwa wanachi wasio na uwezo kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign kutokana na malalamiko kuwa mengi kwani kila pembe kuna malalamiko.

“Tuliona kama Serikali kuna umuhimu wa kuanza na kampeni hii, lakini tunashukuru imetekelezwa vizuri kwa wananchi na niseme kamapeni hiyo inaendelea vizuri na kwa jinsi ilivyopokelewa ni wazi kuwa kuna uhitaji wa msaada wa kisheria hapa nchini,”amesema

Anaeleza hadi sasa tayari kampeni hiyo imefikia wanachi zaidi 383,293 katika mikoa sita, Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu ambapo kupitia kampeni hiyo, migogoro 511 ilitatuliwa na imesaidia nchi kubaini migogoro mingi kwenye jamii.

Anataja maeneo yawaliyoyabaini kuwa na shida zaidi ni ardhi, matunzo ya watoto, ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia.

Kutokana na kubainika kwa hayo, anaitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau kutekeleza kikamilifu utoaji wa msaada wa kisheria kwa mujibu wa sheria.

“Hivyo wale wote wanaoguswa na haki za jamii tunaomba wajitokeze kufanya jitihada hizi hapa tunawekeza kupatikana kwa haki.

Mheshimiwa Jaji Mkuu, umesema ushirikiano katika kujitathmini umebaini mapungufu yetu katika taasisi zetu, nami nakuunga mkono kwenye hilo kama ulivyofanya kwa REPOA, hivyo taasisi zingine zote tushirikiane kubaini mapungufu kwa pamoja ili kurekebisha mapungufu,” anasisitiza Rais Samia.

Vile vile amesistiza kuharakishwa kusikilizwa kwa kesi za biashara, ambapo anasema wanapovutia mitaji na uwekezaji nchini na kufungua fursa za kibiashara wanatambua kwamba uwekezaji unaambatana na masuala ya kisheria na migogoro ya kibishara ni vyema kwa mahakama zetu zitoe umuhimu kwa mashauri ya namna hiyo pia.

“Mheshimiwa jaji Mkuu Ibara ya 107 kifungu (a) kifungo kidogo cha pili mpaka (e) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeweka kanuni za kuzingatia pindi Mahakama inapotoa uamuzi wa mashauri mbalimbali.

Kanuni hizo ni kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu ya kijamii na kiuchumi kutochelewesha haki bila sababu ya msingi, kuukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro na kutenda haki bila kufungwa kupitia kiasi au kasi ya masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamishwa kutenda haki,”amesema.

Anafafanua kuwa unapochukua hatua za usuluhishi unaharakisha kupatikana kwa haki na haileti chungu na maovu.

“Unajua hukumu inaleta chungu na maovu kwa yule anayehukumiwa kwa yule ambaye haki haiendi upande wake, lakini usuluhishi wote wanakubaliana kwa hiyo inaondosha machungu na maovu.

Kwa hiyo ningeomba sana kwamba tuifuate ibara ile ambayo nimeiosoma ambayo ina mambo manne,moja likiwa ni kutenda haki kwa wote,kutochelewesha haki,kutofunga na masharti yakiufundi kupitia au kupita kiasi na kutoa kipaumbele katika usuluhishi,” amesema.